Monday, 24 August 2015

CCM IRINGA MJINI YAJIZATITI KUMNG'OA MCHUNGAJI MSIGWA, WASALITI NA WASIOVAA SARE KUSHUGHULIKIWA
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa kimetoa msaada wa vipaza sauti 18 (horn speakers) kwa chama hicho jimbo la Iringa Mjini ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kampeni za Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Vipaza sauti hivyo vilikabidhiwa jana kwa wajumbe wa halmashauri ya CCM ya Manispaa ya Iringa waliokuwa na kikao maalumu cha maandalizi ya kampeni za uchaguzi huo.

Akikabidhi vifaa hivyo, Katibu wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga alisema vimenunuliwa kwa Sh Milioni 36 zilizotolewa katika mfuko maalumu wa kampeni za chama hicho mkoa wa Iringa.

Alisema kwa kupitia msaada huo kila kata katika jimbo la Iringa Mjini itapata kipaza sauti kimoja kitakachotumika kusaidia kampeni za madiwani, mbunge na rais.

Mtenga alisema CCM inaingia katika uchaguzi huo ikiwa na uhakika wa ushindi mkubwa katika jimbo hilo ambalo kwa miaka mitano iliyopita lilikuwa likiongozwa na Mchungaji Peter Msigwa aliyechaguliwa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Pamoja na matumaini hayo makubwa, Mtenga aliwataka viongozi na wanachama wa chama hicho kufanya kazi ya kisiasa ili lengo hilo litimie.

“Jimbo la Iringa Mjini linawapiga kura zaidi ya 100,000; pamoja na kuwa na mikakati inayotuhakikishia ushindi hatutakiwa kulala, tunatakiwa kuwajua wapiga kura waliko, tuwafuate na tuwaeleze kwanini Mchungaji Msigwa hastahili kurudi tena bungeni,” alisema.

Naye Katibu wa CCM Jimbo la Iringa Mjini, Elisha Mwampashi amesema baada ya mchakato wa kura za maoni kumalizika na uteuzi wa wagombea kufanywa, wapo baadhi ya wana CCM ambao kwa matendo yao wanaonekana kuwa na mipango ya kukisaliti chama hicho.

“Wapo, wengine walikuwa wagombea wa nafasi mbalimbali na wengine ni viongozi na wanachama amabo hatupo nao kikamilifu wakati tukielekea katika uchaguzi mkuu” alisema.

Mwampashi alisema CCM haitakiwa kuwavumilia wanachama wa aina hiyo na akawaomba wajumbe wa halmashauri hiyo kutoa taarifa za wanachama wasaliti ili waweze kushughulikiwa.

Akishukuru kwa msaada huo, Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Iringa, Abeid Kiponza alisema; “vinatakiwa kutumika kwa kazi iliyokusudiwa, na kazi hiyo si nyingine zaidi ya kukiletea ushindi Chama cha Mapinduzi.”

Wakati huo huo, Kiponza amewataka wagombea udiwani, ubunge na viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama hicho kuvaa sare za chama hicho katika kipindi chote cha kampeni.

“Sitaki mavazi yenu ya disco, na mgombea au kiongozi anayeogopa kuvaa sare za chama, akae nyumbani kwake,” alisema katika kikao hicho ambacho pia waliokuwa wagombea udiwani na kuuanguka katika mchakato wa kura za maoni walitangaza kuvunja makundi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment