Wednesday, 26 August 2015

BENKI YA MUCOBA YAENDELEA KUJIIMARISHA KIMTAJI, HISA ZAKE ZAGOMBANIWA

BENKI ya Mucoba PLC inaendelea kuimarisha mtaji wake ili kuboresha utendaji na huduma inazotoa kwa wadau wake mbalimbali ndani na nje ya mkoa wa Iringa.

Benki hiyo ya kijamii ya kwanza kuanzishwa nchini, miaka 15 iliyopita, ina mtaji wa Sh Milioni 828 na kwa mujibu wa sheria zinazosimamia benki inatakiwa kuwa na mtaji wa Sh Bilioni 2 ili iendelee kutoa huduma zake.

“Tumeingia katika soko la hisa la Dar es Salaam kama moja ya mkakati wetu wa kuongeza mtaji; na uuzaji wa hisa  toleo la awali umeshazinduliwa katika wilaya zote za mkoa wa Iringa,” Mwenyekiti wa Bodi ya benki hiyo, Attilio Mohole alisema katika mkutano mkuu wa 16 wa wanahisa wa benki hiyo uliofanyika mjini Mafinga hivikaribuni.

Mohele alisema hisa zinazouzwa kama toleo la awali ni hisa Milioni 20 zenye thamani ya Sh Bilioni 5 zinazouzwa kwa Sh 250 kwa hisa moja.

Pamoja na changamoto ya mtaji, Mohele alisema benki imeendelea kutoa huduma zake kuu za akiba na mikopo kwa kuongeza ufanisi uliowezesha akiba za wateja wake kuongezeka kutoka Sh Bilioni 10.2 hadi Sh Bilioni 11.4.

Wakati akiba ikiongezeka, mwenyekiti huyo alisema mikopo ilipungua kutoka Sh Bilioni 7.8 hadi Sh Bilioni 7.4.

Meneja wa benki hiyo, Ben Mahenge alisema sambamba na huduma hizo benki hiyo inaendelea kutoa huduma nyingine ambazo ni pamoja na utumaji fedha, bima na matumizi ya teknolojia.

Kutokana na shughuli zake hizo, Mahenge alisema mwaka 2014 benki ilipata faida ya Sh Milioni 450 kabla ya kodi tofauti na Sh Milioni 293 ilizopata mwaka 2013.

“Kutokana na faida ambayo benki imepata mwaka 2014, bodi ya wakurugenzi imependekeza kila mwanahisa apate gawio la Sh 40 kwa hisa lenye thamani ya Sh Milioni 57.7 ambayo ni sawa na asilimia 28 ya faida ya benki baada ya kodi,” alisema.

Ili kufikisha huduma jirani na wananchi pamoja na kuimarisha vyama vya kuweka na kukopa, Mahenge alisema Mucoba itaendelea kuanzisha vituo vidogo vya utoaji huduma katika maeneo ya vijijini.

Alisema kwasasa benki inatoa huduma katika mkoa mzima wa Iringa na Madibira wilayani Mbarali mkoani Mbeya.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment