Sunday, 1 February 2015

VODACOM WAMTEMBELEA NA KUMCHUKUA BINTI WA KILOLO ALIYESHINDA MILIONI 100 ZA PROMOSHENI YA JAYMILIONI

Meneja Uhusiano wa Umma  wa Vodacom, Matina Nkurlu na Mkuu wa Kanda ya Kusini Magharibi wa kampuni hiyo Amos Vuhahula (katikati) wakimsalimu mshindi wa droo ya 14 ya Jaymilioni, Uwezo  Magendenye (kushoto) aliyejinyakulia milioni 100
Uwezo wakionesha mazingira ya nyumbani kwao kijijini kwake Pomerini, wilayani Kilolo mkoani Iringa
Hapa akionesha namna anavyoshiriki kazi za nyumbani za kila siku
Akiwa katika hali ya furaha baada ya kutembelewa na maafisa wa Vodacom
Hapa ndipo alipokuwa anafanya kazi kabla ya kuibuka mshindi wa droo hiyo
Mazingira halisi ya nyumbani kwao
Baba yake mzazi, Alatanga Magendenye
MSHINDI wa kwanza wa Sh Milioni 100 katika droo ya 14 ya promosheni ya Jaymilioni inayoendeshwa na kampuni ya mawasiliano ya Vodacom, amekutana na maafisa wa kampuni hiyo kijiji kwake Pomerini, wilayani Kilolo mkoani Iringa ikiwa ni siku mbili tangu aibuke na ushindi huo.

Mshindi huyo Uwezo Magendenye (22) hakuamini macho yake na furaha yake ya ushindi huo ilidhihiri zaidi baada ya kukutana na Meneja Uhusiano wa Umma  wa Vodacom, Matina Nkurlu na Mkuu wa Kanda ya Kusini Magharibi wa kampuni hiyo Amos Vuhahula.

Baada ya kufanya maongezi naye pamoja na familia yake, maafisa hao wa Vodocam waliondoka na binti huyo hadi mjini Iringa ambako maandalizi ya safari ya kuelekea Dar es Salaam atakakokabidhiwa rasmi kitita hicho, yanafanyika.

 “Baada ya kusikia kuna mtu kashinda Sh millioni moja, nikajiuliza huyu anatokea nchi gani? nikagundua ni mtanzania kama mimi, nikapata hamasa zaidi ya kushiriki kwa kutuma neno “JAY” Kwenda namba 15544,” Magendenye alisema.

Alisema; “ilikuwa Januari 29 majira ya saa 6 mchana nilipopokea ujumbe mfupi …sms…unaoashiria kuwa mimi ni mshindi wa shindano na baadae nikapigiwa simu.”

Alisema amepata bahati ya kuibuka na mamilioni hayo ikiwa ni wiki mbili tu tangu aanze kufanya kazi kama mhudumu wa mapokezi katika nyumba ya kulala wageni ya Luganga Lodge iliyopo mjini Kilolo, wilayani Kilolo.

 “Sikuamini na hata baadhi ya marafiki zangu hawakuamini, walianza kunipigia simu baadhi yao wakitaka kujua kama waliochosikia ni kweli, na hata nilipothibitisha ni kweli na kwamba nimewasiliana na Vodacom wengine hawakuamini,” alisema.

Pamoja na hayo yote alisema yeye ndiye mshindi wa droo hiyo na roho yake imetulia na kuona ni jambo lisilo na shaka tena baada ya kutembelewa na maafisa hao wa Vodacom nna kumchukua tayari kwa ajili ya safari ya kwenda kukabidhiwa kitita hicho.

Baba wa mshindi huyu, Alatanga Magendenye (70) alieleza kufurahishwa kwake juu ya ushindi wa binti yake na kusisitiza kwamba hatapenda kumuingilia kwenye matumizi ya pesa hizo japokuwa kama mzazi angependa kuona binti yake huyo anapata elimu bora.

Naye mama mzazi wa binti huyo Delfina Kisoma (64) alielezea furaha yake juu ya ushindi wa binti yake huyo akisema ni matarajio yao ushindi huo utasaidia kubadili maisha ya binti huyo na familia yao.

Akizungumza namna fedha hizo zitakavyobadili maisha yake, binti huyo alisema atajiendeleza kielimu ili kutimiza ndoto yake ya kuelimika vizuri ambayo hata hivyo hakuweza kuifikia kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya uwezo mdogo wa kifedha wa wazazi wake.

“Ndoto yangu ya kurudia mitihani ya kidato cha nne iliyokufa miaka miwili iliyopita kutokana na uwezo mdogo wa familia sasa imefufuka. Nitarudi shule, nitasoma kwa bidii hadi nipate shahada ya chuo kikuu kama itawezekana,” alisema.

Alitaja matumizi mengine atakayofanya kuwa ni pamoja na kununua ardhi na kupanda miti, kukarabati nyumba ya wazazi wake na kusaidia ndugu zake ambao wanauhitaji wa kusoma.

“Katika maisha yangu nimeishapitia mambo mengi nahangaika na maisha hadi kufikia hapa nilipo nikiwa mhudumu kwenye nyumba ya wageni. Kwa ushindi huu naamini nitafungua shughuli zangu za biashara ikiwemo kuanzisha biashara ya  maduka ya M-Pesa pia kufungua  nyumba yangu ya kulala wageni,” alisema

Aliongeza kuwa kwa muda mrefu amekuwa akishiriki kwenye promosheni mbalimbali na hajawahi kufanikiwa kwa ushindi huu anaamini kuwa promosheni hizi hususani za Vodacom ni za kweli na amewataka  wateja wote kushiriki ili kutopoteza bahati zao za kujishindia mamilioni ya fedha na kubadilisha maisha yao.

Meneja Uhusiano wa Umma  wa Vodacom, Nkurlu amempongeza mshindi na kuwahimiza wateja wote kuchangamkia promosheni hiyo kwa kuhakikisha wanatuma neno JAY kwenda namba 15544 ili kutopoteza nafasi zao za kushinda.

Aliitaja njia nyingine ya kushinda kuwa ni kutuma neno AUTO kwenda namba 15544 iwapo simu haina fedha ambapo  mteja akiweka fedha anakatwa shilingi 300/-

Alisema tangu promosheni hiyo ianze mapema mwezi uliopitau tayari wateja 2  wamekwishajishindia milioni 10 na wateja watano wameishajishindia shilingi milioni moja kila mmoja  na  maelfu wengine tayari wamejishindia muda wa maongezi.

“Promosheni hii itadumu kwa muda wa siku mia moja, bado kuna mamilioni ya fedha yanawasubiri watanzania, wanachopaswa kufanya ni kuhakikisha  kila siku wanaangalia kama namba zao zimeibuka na ushindi kwenye droo ya siku kwa kutuma neno Jay kwenda namba 15544.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment