Thursday, 5 February 2015

MKUU WA MKOA WA IRINGA ACHUNGUZA MATUMIZI YA MAGARI YA UMMA KWA SHUGHULI BINAFSI ZA MAAFISA WA SERIKALI


MKUU wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza ameahidi kulifanyia kazi suala la watumishi wa umma wanaotumia magari ya serikali kwa shughuli zao binafsi na baada ya muda wa kazi kwisha.

Alitoa ahadi hiyo hivikaribuni baada ya mtandao huu kutaka kujua ni hatua gani zinachukuliwa na serikali kwa watumishi wanaotumia rasilimali za umma yakiwemo magari kwa maslai yao binafsi.

“Naomba hilo mniachie kwanza, nitalifanyia uchunguzi na nitawaletea majibu wakati wowote kuanzia sasa,” alisema bila kutoa ufafanuzi zaidi.

Swali hilo liliulizwa likilenga kutoa majibu ya kilio cha wananchi wanaowalalamikia baadhi ya maafisa wa serikali kutumia magari ya umma kwa shughuli zao binafsi ambazo nyingine hufanywa katika muda wanaotakiwa kuwa kazini.

“Moja ya sababu ya kuwakosa maafisa hao maofisini na kuathiri mahitaji ya jamii ni haya magari wanayopewa kwa shughuli za umma,” alisema mmoja wao ambaye hata hivyo hakutaka kutaja jina lake.

Alisema wamekuwa wakiwaona maafisa hao wakiwa na magari hayo sehemu za starehe zikiwemo Bar, mashambani na kwenye miradi yao mbalimbali ikiwemo miradi ya ujenzi yakitumika kwa shughuli zao binafsi ikiwemo kubeba mikaa na mizigo mingine.

Alisema miaka kadhaa iliyopita, walisikia tangazo la serikali likipiga marufuku matumizi ya magari hayo kwa shughuli binafsi na baada ya muda wa kazi bila kibali maarufu.

“Hatujui utaratibu huo uliishia wapi, kwanini ulianzishwa na nani aliyeuuwa nani, mbona magari haya yanayonunuliwa kwa kodi zetu yanatumiwa kufanya kazi binafsi za watumishi wa serikali?” aliuliza.

Novemba mwaka jana, Rais Jakaya Kikwete alionesha kukerwa na tabia na mienendo ya watumishi wa umma wasiozingatia kanuni na sheria za utendaji kazi katika kuwahudumia wananchi na katika shughuli zingine za serikali, hali ambayo anasema inarudisha nyuma maendeleo ya nchi na ukuaji wa uchumi.

Rais aliyasema hayo wakati akizindua Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 10 ya Utumishi wa Umma yaliyohudhuriwa na watumishi wa umma wa kada mbalimbali.

Mtumishi wa umma ni mtu aliyeajiriwa ndani ya Mamlaka ya Serikali ambaye anatakiwa kufanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Na.8 ya mwaka 2003 na kanuni zake. Rais alisema amekuwa akikwazwa na baadhi ya mambo yanayofanywa na baadhi ya watumishi wa umma kama rushwa, uzembe na matumizi mabaya ya madaraka.

Alisema vitendo hivyo vinawaaminisha wananchi kuona utumishi wa umma kama ni ukwamishaji wa maamuzi na kuwataka watumishi wa umma kujitazama upya ili utumishi wa umma usionekane kama ni kikwazo na badala yake uwe ni uwekezaji na kuharakisha maendeleo ya nchi na kukuza uchumi wake.


Kwa ujumla, Rais hakufurahishwa na uwajibikaji mbovu uliopo nchini katika kada ya utumishi wa umma ambayo ndiyo moyo wa utendaji wa kazi za kila siku serikalini.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment