Sunday, 8 February 2015

MKURUGENZI WA TIGO AKUBALI KUBEBA SEHEMU YA MZIGO WA WANANCHI WA KUCHANGIA UJENZI WA SHULE KALENGA

Mkurugenzi wa Kampuni ya Tigo Nyanda za Juu Kusini, Jakson Kiswaga (kushoto) akikabidhi kwa mkuu wa shule ya msingi Kipera, Sista Clementina Msungu moja kati ya bati 70 alizochangia kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu
Mwenyekiti wa kijiji, Francis Yangi
Mwalimu Mkuu, Sista Clementina Msungu

Kiswaga mwenyewe akifafanua umuhimu wa kuchangia maendeleo
Baadhi ya wananchi waliohudhuria
MKAZI wa Kalenga, wilayani Iringa mkoani Iringa Jackson Kiswaga amebeba sehemu ya mzigo uliokuwa ubebwe na wananchi wa kijiji cha Kipera kwa kuchangia bati 70 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa nyumba za walimu za shule ya msingi ya kijiji hicho.

Kiswaga ambaye pia ni Mkurugenzi wa Nyanda za Juu Kusini wa Kampuni ya Simu ya Mkononi ya Tigo, alitoa msaada huo jana, katika hafla iliyohudhuriwa na wananchi wa kijiji hicho, walimu na wafanyakazi wa shule hiyo.

Msaada huo wenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni 1, umeipa nafuu nguvu kazi ya kijiji hicho dhidi ya mzigo wa kuchangia maendeleo ya shule hiyo.

Akishukuru kwa msaada huo, mwenyekiti wa kijiji hicho Francis Yangi alisema kati ya wakazi 2,339 wa kijiji hicho, 550 wana uwezo wa kufanya kazi na kwa mujibu wa taratibu za kijiji wanalazimika kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo .

“Kama ndugu yetu Kiswaga asingetoa msaada huo, kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi katika kijiji hichi angelazimika kuchangia Sh 2,000 ili shule hiyo ipate bati hizo sabini,” alisema na kumpongeza kwa kuwasaidia kubeba mzigo huo.

Akikabidhi msaada huo, Kiswaga alisema aliahidi kuchangia ujenzi wa nyumba za walimu wa shule hiyo alipoalikwa kwenye mahafali ya shule hiyo Septemba mwaka jana.

“Wito wangu kwa wadau wengine wa maendeleo, turudishe kidogo tunachopata kwa kuchangia shughuli za maendeleo ya nchi yetu,” alisema na kusisitiza umuhimu wa elimu kwa maendeleo ya Taifa.

Alisema shule za vijijini zina upungufu wa vifaa mbalimbali ikiwemo miundombinu yake na akatoa wito kwa watanzania wengine kuona kwamba wana wajibu wa kusaidia watu wengine pale wanapopata fursa.

Awali Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Clementina Msungu alishukuru kwa msaada huo na kuahidi kuutumia kwa lengo lililokusudiwa.

Alisema mbali na ni kuhitaji msaada wa bati kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu, shule hiyo pia inahitaji msaada toka kwa wadau kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wanafunzi wenye ulemavu.

“Shule hii ina wanafunzi 644 na kati yao wanafunzi 66 ni walemavu ambao mahitaji yao ni makubwa ili waweze kufanya vizuri kimasomo,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment