Thursday, 5 February 2015

JAJI SHANGALI AHOFIA VIKWAZO NA GHARAMA ZA ADA NA MALIPO YA MAWAKILI KUWANYIMA WANANCHI FURSA YA KUPATA HAKI

Jaji Mary Shangali
Akikagua gwaride maalumu wakati wa maadhimisho ya siku ya sheria nchini, mjini Iringa
Wakili wa Serikali Mfawidhi, Abel Mwandalama
Wakili Lwezaula Kaijage, mwakilishi wa TLS
Burudani za nyoka zilikuwepo
Baadhi ya waalikwa walioshiriki maadhimisho hayo
Kwaya nayo ilikuwepo
Mchezo wa kuchezea kofia
JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mary Shangali amesema serikali ina wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kimahakama bila vikwazo vya kiufundi wala gharama kubwa za ada au malipo ya mawakili.

Shangali aliyasema hayo kwenye sherehe ya kuadhimisha siku ya sheria nchini iliyofanyika mahakamani hapo juzi.

Mbele ya waalikwa mbalimbali wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa na madhehebu ya dini, alisema serikali inapokubali kupitisha au kuwepo sheria zenye vikwazo au masharti mengi kama zilivyo baadhi ya sheria za uchaguzi inawanyima wananchi fursa ya kupata haki zao.

Akitoa mfano alisema kutungwa kwa kifungu cha sheria kilichomtaka mlalamikaji katika kesi ya uchaguzi kuweka mahakamani dhamani ya Sh Milioni 5 kabla kesi haijapokelewa na kupangiwa tarehe ya kusikilizwa kilionekana kuwafungia walalamikaji mlango wa kupata haki.

Jaji huyo alisema serikali ina wajibu wa kuhakikisha huduma ya kimahakama inapatikana karibu na wananchi au kwa maeneo mengine wanaifikia kwa urahisi na kwa gharama nafuu.

Alisema kuondolewa kwa vikwazo au masharti mengi ya kupata haki na uwepo wa mahakama huru na imara utasaidia kulinda demokrasia na utawala wa sheria kwa kuzingatia Katiba.

Katika utekelezaji wa kuboresha huduma ya utoaji haki, aliishukuru serikali akisema imeendelea kuzipitia na kuziboresha sheria na hivi karibuni imeanzisha mifumo ya huduma ya msaada wa kisheria ili kusaidia wananchi wanaohitaji msaada wa kisheria kulingana na uwezo wao wa kipato.

“Serikali imeendelea kuzipitia sheria zinazohusu uendeshaji na mwenendo wa kesi ili kuondoa vikwazo vinavyozuia upatikanaji wa haki na ili kuongeza idadi ya wataalamu, vyuo mbalimbali vyenye mikondo ya sheria vimeanzishwa,” alisema.

“Aidha serikali iliazimia kuiondoa mahakama ya Tanzania katika wingu la muda mrefu la bajeti finyu na kuanzisha mfuko maalumu wa mahakama. Kitendo hicho kinaelekea kufanikisha mabadiliko na maboresho yanayofanywa na mahakama ya Tanzania,” alisema.

Awali Wakili wa Serikali Mfawidhi, Abel Mwandalama alisema ili nchi iwe na amani na utulivu ni wajibu wa serikali kama mtendaji mkuu, kusimamia vizuri sheria na kutekeleza maagizo ya bunge na mahakama.

“Katika kutekeleza wajibu huo serikali haina budi kutenda haki kwa wananchi wake wote bila upendeleo wowote,” alisema.

Alisema kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanyika barani Afrika imebainika kuwepo kwa uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu kwenye mchakato mzima wa mfumo wa haki jinai ikilinganishwa na mfumo wa haki madai.

Naye Mwakilishi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Lwezaula Kaijage ili kuwasaidia wananchi wasiojiweza chama hicho kimeanzisha utaratibu wa kutoa msaada wa kisheria bure.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment