Friday, 6 February 2015

CCM IRINGA WAHOFIA UCHAGUZI WA UBUNGE JIMBO LA IRINGA MJINI
IKIWA imebaki miezi tisa kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani Chama cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya Iringa kimejipanga kusimamia ipasavyo Katiba, Kanuni, Taratibu na miongozo yote ya chama ili mikakati yake ya kulirejesha jimbo la Iringa Mjini katika himaya yake ifanikiwe.

Kwa mwaka wa tano sasa, jimbo hilo linaongozwa na Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) aliyeshinda kwa tofauti ya kura 828 katika Uchaguzi Mkuu wa 2010 baada ya kujipatia kura 17,744 dhidi ya kura 16,916 alizopata mgombea wa CCM, Monica Mbega.

Katika kikao hicho kilichohusisha kamati za siasa za kata zote za manispaa ya Iringa, viongozi wa wilaya na baadhi ya viongozi wa mkoa wa Iringa, hofu ya kulirejesha jimbo hilo kama mambo yanayoonekana kufanyika ndivyo sivyo yataendelea, ilidhihirika wazi wazi.

Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na wanaotajwa kutaka kugombea ubunge katika jimbo hilo kuanza kampeni kinyume na katiba ya CCM.

Baadhi ya wagombea hao wameelezwa katika kikao hicho kwamba badala ya kusaidia kukijenga chama ili kukiongezea kuaminika kwa wananchi wa jimbo hilo, wamekuwa wakijijenga wao kwa kutumia taswira inayowachafua wana CCM wengine na chama hicho.

Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Iringa, Elisha Mwampashi alisema; baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya hawana mahusiano tena kwasababu ya harakati za wagombea hao.

Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Iringa, Dk Yahaya Msigwa alisema  CCM imefanya mengi kwa maendeleo ya jimbo hilo na nchi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita lakini cha kushangaza kazi ya kuyasema hayo kwa wananchi imeachwa kwa baadhi ya viongozi.

“Kukaa kwetu kimya kumewafanywa baadhi ya wana CCM wawe kama ndumilakuwili kwa maana ya kwamba mchana anakuwa CCM na usiku anakuwa upinzani,” alisema na kuongeza kwamba kama hawatajirekebisha na mzaha huo inaweza kuwa kazi ngumu kulikomboa  jimbo hilo.

Naye Katibu wa Uchumi na Mipango, Lazalo Manila aliwataka wote wanaotuhumiwa kukiweka chama katika hatari ya kukosa umoja na mshikamano wajirekebishe wakati chama hicho kikielekea kutekeleza mikakati ya kulirejesha jimbo hilo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Iringa aliwataka wanaotafuta ubunge katika jimbo hilo wasikijeruhi chama na kukisababishia ugonjwa usiotibika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

“Wapo baadhi yao wanatafuta ubunge kwa kukibomoa chama; kila siku wanafanya vikao feki na kwa bahati mbaya vikao hivyo havielekei kuwa na manufaa ya maana kwa chama badala ya kuongeza mpasuko,” alisema.

Bila kuwataja majina, Kiponza alisema katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliopita upo ushahidi unaoonesha walishindwa katika baadhi ya mitaa kwasababu baadhi ya wana CCM waliamua kupeleka nguvu zao upinzani na walifanya hivyo ili kuwakomoa wana CCM wenzao wanaokubalika katika maeneo hayo.

Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Mtenga alihitimisha hofu hiyo kwa kutoa miezi miwili kwa kamati ya siasa ya manispaa hiyo kuyafanyia kazi mambo yote yanayokihatarisha chama hicho na mikakati yake ya kulirejesha jimbo hilo mikononi mwake.

Aliitaka kamati hiyo kuonesha meno yake kwa kutumia Katiba, Kanuni na Taratibu zingine za chama kuyashughulikia yale yote yanayosaliti chama kwa ili kurejesha imani kwa wapiga kura wake wote.

“Ukiwa mtendaji lawama ya kwanza utakayopata ni pale unaposimamia taratibu za kikatiba zinazooneka kuwaathiri watu wengine. Lakini ili chama kiende ni lazima tusiogope lawama hizo,” alisema.

Alisema jimbo la Iringa Mjini litarudi mikononi wa CCM kama mchakato mzima wa mkakati huo utafanyika kwa misingi ya Katiba, taratibu na haki.

Alisema wapo baadhi ya wana CCM ambao wamekuwa kikwazo katika harakati hizo na hata kudiriki kumsukia zengwe la kutaka ahamishwe kwasababu tu anafanya kazi za CCM kwa mujibu wa taratibu.

Bila kuwataja majina, Mtenga alisema kuna vijana wanne ambao wamepewa pikipiki ya kuzunguka huku na kule kuawashawishi wanachama kuungna mkono hoja yao ya kutaka aamishwe ili wapate fursa nzuri ya kuvunja taratibu za chama.

“Wapo wasiotaka kufuata taratibu na katika kuhalalisha mambo yao wamekuwa wakinihusisha na mambo ya uzushi yanayolenga kunichafua, vita yangu dhidi yao ni kusimamia haki na mkakati wa ushindi wa CCM,” alisema na kuongeza kwamba CCM inaweza kupata ushindi wa kishindo kama wana CCM watafanya kazi ya chama badala ya kutumiwa kufanya kazi ya wagombea.

Alisema CCM inatakiwa kukitumia kipindi kilichobaki kabla kipenga cha mchakato wa uchaguzi mkuu hakijapigwa kujenga chama ili kuifanya kazi iliyoko mbele yao ya kulirejesha jimbo hilo iwe rahisi.

“Wakati sisi tunahangaika kuwajenga watu, wenzetu wa Chadema wanaendelea kukijenga chama chao. Kila walipo watu wawili ili mradi kuna Chadema mmoja lazima kutakuwa na maongezi ya kukisifia chama hicho,” alisema.

Alisema kama wanataka kushinda katika uchaguzi huo ni lazima warudi kwenye mstari ambao msingi wake mkubwa ni Katiba.

Mtenga aliwataja watu wawili kwa jina moja moja la Alex na Clara kwamba ni vinara wa kushawishi watu kufanya kazi za wagombea badala ya kazi za chama na kwamba wanatakiwa kufikishwa katika kamati ya maadili ya maadili.

Alisema wamepokea ushahidi kupitia vinasa sauti unaonesha wawili hao kwa nyakati tofauti wakipita maeneo mbalimbali ya jimbo la Iringa mjini wakifanya kazi inayowakera wana CCM wengine na hivyo kuhatarisha umoja wake.

Pamoja na wawili hao, Mtenga aliitaka kamati ya siasa ya wilaya kushirikiana na viongozi wa ngazi zote katika jimbo hilo ili kuwabaini na kuwachukulia hatua wale wanaokihujumu chama katika kipindi alichokiita ni muhimu kwa wanaCCM kuwa kitu kimoja dhidi ya mapambano ya kuing’oa Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Katibu wa CCM wa Manispaa ya Iringa, Zongo Lobe Zongo alisema kamati yake haitakuwa na huruma tena kwa watu wote wanaotuhumiwa kukivuruga chama.

“Tutawaita wanaotuhumiwa sasa na tutafanya uchunguzi na kushughulikia malalamiko mengine yote yanayowahusu wote wasiofuata taratibu,” alisema.

Wana CCM waliotangaza nia ya kuwania jimbo hilo mpaka sasa ni pamoja na Jesca Msambatavangu na Frank Kibiki, na wengine wanaotajwa kutaka kujitosa ni Frederick Mwakalebela, Mahamudu Madenge, Dk Yahaya Msigwa, Zakaria Hanspope, Salim Asas na Nuru Hepautwa. 

Habari kwa kina kuhusiana na mkutano huo utaletewa hivi punde………………………..

Reactions:

0 comments:

Post a Comment