Saturday, 10 January 2015

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KUAJIRI WAHITIMU WA JESHI LA KUJENGA TAIFA


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mahamudu Mgimwa akigagua kikosi cha wahitimu hao
Akiwa katika picha ya pamoja na makamanda wa JKT
VIJANA wa kujitolea wanaomaliza mafunzo ya awali ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wataendelea kuajiriwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia mikakati yake ya kukabiliana na ujangili katika hifadhi zake za Taifa.

Naibu Waziri wa Maliasilia na Utalii, Mahamudu Mgimwa alisema mpango huo unalenga pia kushughulikia changnamoto ya upungufu wa askari wa wanyamapori katika hifadhi hizo na mapori ya akiba.

Mgimwa aliyasema hayo kwenye hafla ya kuhitimisha mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria kwa kundi la miaka 50 ya Muungano awamu ya pili yaliyofanyika katika viwanja vya kikosi 841 KJ Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa, hivikaribuni.

Alisema wizara inataka kuwaajiri vijana hao kwa kuzingatia kwamba moja ya mambo muhimu waliyojifunza katika mafunzo yao ya miezi mitatu ni uzalendo.

“Ndani ya uzalendo kuna mambo mengi ya msingi tunayojifunza ikiwa ni pamoja na kujilinda, malezi mema na kujiajiri katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo na ufugaji. Ulinzi ni wa watanzania wote na malezi ni jambo muhimu kwasababu linasaidia kulinda maadili ya taifa na ya mtanzania,” alisema.

Alisema serikali imetengeneza mkakati unaolenga kuwapa ajira vijana wa kujitolea wanaomaliza mafunzo ya JKT katika vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama.

“Mwaka jana tumeajiri vijana 489 kati yao asilimia 50 wametoka JKT na asilimia 50 wengine wametoka katika vyuo vyetu. Mwaka huu tutaajiri vijana wengine 500 kwa mgawanyo huo huo,” alisema.

Katika risala yao iliyosomwa Godwin Mbise, wahitimu wa mafunzo hayo walisema kwa kupitia mafunzo hayo wamefundishwa ukakamavu na kushiriki vyema katika mazoezi mbalimbali yaliyoendeshwa kama ulengaji wa shabaha, mafunzo ya kivita porini na mafunzo ya elimu rika na uzalendo.

Wakizungumzia changamoto walizokutana nazo katika kipindi chote cha mafunzo yao, wahitimu hao walisema kulikuwepo na upungufu wa baadhi ya sare vikiwemo viatu (raba na buti) pamoja na kofia uliosababisha ushiriki wao katika mafunzo hayo kuwa katika mazingira magumu.

Pamoja na kuimba serikali kushughulikia changamoto hiyo, wahitimu hao wameomba muda wa mafunzo hayo uongezwe kutoka miezi mitatu hadi zaidi ya miezi sita ili wapate ujuzi wa kutosha.


Akitoa taarifa ya vijana hao , Mkuu wa Kikosi cha 841 KJ Luteni Kanali Martini Mkisi ameipongeza serikali kwa kurejesha JKT kwa kuwa itajenga uzalendo kwa vijana kuipenda nchi yao huku Mwakilishi wa Mkuu wa JKT nchini Kanali Menas Mbele akiwaasa vijana hao kutokukubali kurububiwa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment