Friday, 2 January 2015

WAZEE WASIOJIWEZA WASUSA KULA SIKU MBILI WAKIMLILIA RC MASAWE


WAZEE wasiojiweza na watoto yatima walioko katika Kituo cha Kiilima kilichoko Bukoba Vijijini, wamesema walilazimika kususa kula kwa siku mbili mwezi uliopita baada ya kupata habari za kuondolewa kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Massawe.

Walitoa kauli hizo juzi wakati wakipokea zawadi za mwaka mpya, walizokabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongella aliyechukua nafasi ya Massawe kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete.

Evelyn Mshana ambaye ni mmoja wa wahudumu kituoni hapo, alisema mwezi uliopita wahudumu wa kituo hicho walijikuta katika wakati mgumu baada ya wazee kumi na watoto yatima 12 wanaolelewa hapo, kususa kula na kububujikwa na machozi wakimlilia Massawe ambaye anasubiri kupangiwa majukumu mengine na Rais Jakaya Kikwete.

“Siku ya kwanza, baada ya kupita saa tano tangu watangaze kutokula wala kunywa chochote, uongozi wa kituo uliamua kukaa nao na baada ya kuwahoji, walisema wamesikia kupitia vyombo vya habari kuwa mtu wao ameondoka, hivyo wako kwenye huzuni.

“Jambo hilo sisi tuliliona la kawaida sana, lakini madhara yake yalikuwa makubwa, unawaona wazee hawa wengine wana miaka zaidi ya 90 waliendelea na msimamo wa kutokubali kula chakula wala kunywa chochote kwa siku mbili, tuliendelea kupata wakati mgumu mpaka tulipowabembeleza sana na kuwaahidi kuwasiliana na mkuu wa mkoa huyo wa zamani ili amshauri mkuu wa mkoa mpya aendelee kuwatembelea na kuwatafutia misaada sambamba na kuibua miradi itakayowasaidia kama alivyokuwa akifanya Massawe,” alisema Evelyn.

Mmoja wa wazee aliyeishi kituoni hapo kwa zaidi ya miaka 25, Everister Kayogera, alipoulizwa sababu za kugoma kula na kuangua vilio kituoni hapo, alisema Massawe alikuwa ni nguzo kubwa kwao kwani aliwashauri mambo mengi ambayo yamewanufaisha kwa kipindi kifupi.

“Tunamshukuru Rais kwa kutukumbuka kila mwaka na kututumia zawadi za mwaka mpya, kwanza tuliposikia kuwa mkuu wetu wa mkoa Massawe amehamishwa tuliumia sana mpaka machozi yakatutoka huku tukiamua kulala njaa na kushinda njaa mpaka aje tuongee naye, aweze kutuhakikishia kama yale tuliyopanga naye yataendelea kutekelezeka,” alisema Kayogera.

Mzee mwingine ambaye pia ni mlemavu wa viungo, anayelelewa kituoni hapo, Wilson Zikumana alisema kwa takribani miaka mitatu sasa, Massawe aliwabadilishia mfumo wa maisha, kiasi cha kuwafanya wajishughulishe na kufanya shughuli za uzalishaji, ikiwa pamoja na kilimo ambacho kinawawezesha kujitegemea kwa kiasi kikubwa kwa chakula.

Alisema walikuwa pia na mipango mingi, ikiwa ni pamoja na kuanzisha ufugaji. Kutokana na hali hiyo, walimshauri Mongella kuhakikisha anafika kituoni hapo mara kwa mara na kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili hasa ya ukosefu wa huduma ya afya.
chanzo;habarileo.co.tz

Reactions:

0 comments:

Post a Comment