Monday, 5 January 2015

UTITIRI WA WAGOMBEA URAIS WA CCM USIWAOGOPESHE, CCM KUJA NA MGOMBEA KIBOKO YAO-PROFESA MSOLLA


 
Profesa Msolla katika mkutano wake na vijana wa kijiji cha Mbigili, Kilolo
Katika hotuba yake
Akapokea maswali 

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kilolo mkoani Iringa, Profesa Peter Msolla amewataka watanzania kutohofia utitiri wa wana CCM waliotangaza nia na wanaotajwa kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Hivi karibuni akiwa katika kijiji cha Mbigili katika ziara yake ya kila mwaka ya kutembelea vijiji vyote 106 vya jimbo hilo kwa lengo la kukagua shughuli za maendeleo, Profesa Msolla alisema CCM itafanya kila iwezalo kuwaletea mgombea anayekubalika ndani na nje ya chama.

“Mtawasikia wengi wakijitokeza na yatazungumzwa mengi juu yao, lakini CCM ni chama chenye utaratibu mzuri, huenda kuliko vyama vingine vyote nchini wa kumpata mgombea wake; utaratibu huo ndio utakaotumika kumpata mgombea huyo mwaka huu,” alisema.

Baadhi ya wanaCCM ambao tayari wamatengaza nia ya kuwania nafasi hiyo ya juu kabisa ya uongozi nchini ni pamoja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, Mbunge wa Nzega Dk Hamis Kigwangalla, Waziri wa Maliasilia na Utalii Lazaro Nyalandu na Waziri Mkuu Mizengo Pinda anayedai kutangaza nia hiyo kimyakimya.

Wengine wanaotajwatajwa kuutaka uraia kupitia chama hicho ambao hata hivyo hajatangaza rasmi nia hiyo ni pamoja na mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.

Wapo pia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Waziri wa Katiba na Sheria Dk Asha Rose Migoro.

Wengine ni pamoja na mbunge wa Sengerema William Ngeleja na mbunge wa Songea Mjini Dk Emanuel Nchimbi ambao kwa pamoja wamewahi kuwashika nafasi za uwaziri katika serikali ya awamu ya nne, kabla ya uteuzi wao kutenguliwa.

Wakati Ngeleja aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Nishati na madini kabla ya kupandishwa na kuwa waziri kamili wa wizara hiyo, Dk Nchimbi naye aliwahi kuwa naibu waziri wa mambo ya ndani kabla hajateuliwa kuwa waziri kamili wa wizara hiyo.

Akizungumzia utaratibu wa kumpata mgombea mmoja atayepeperusha bendera ya CCM dhidi ya wagombea wengine wa vyama vya upinzani, Profesa Msolla alisema mchujo wa majina hayo uanzia ngazi ya kamati kuu, halmashauri kuu na hatimaye mkutano mkuu unaopitisha jina moja.

“CCM ni lazima italeta mgombea mwenye sifa kwasababu inatambua, urais ni taasisi nyeti; akipelekwa mtu asiye na sifa za kutosha anaweza kuliingiza taifa kwenye matatizo makubwa,” alisema.

Muda utakapofika, Profesa Msolla aliwasihi watanzania kumpigia kura mgombea atakayepitishwa na mkutano mkuu wa taifa wa CCM ambaye pamoja na mambo mengi atahakikisha Taifa linaendeshwa kwa misingi ya haki na amani.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment