Saturday, 10 January 2015

RAIS, WAZIRI MKUU KUPIGIWA MAGOTI UJENZI WA BARABARA YA IRINGA HIFADHI YA RUAHA KWA KIWANGO CHA LAMI


KIKAO cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Iringa kimeunda timu maalumu itakayokutana na Waziri Mkuu Mzengo Pinda au Rais Jakaya Mrisho Kikwete ili kuwasilisha ombi maalumu litakalowezesha barabara ya Iringa Mjini hadi Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ijengwe kwa kiwango cha lami, haraka iwezekanavyo.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 104 ipo katika ahadi za uchaguzi zilizotolewa na Rais Kikwete katika Uchaguzi Mkuu wa 2010 ambazo hazipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

“Mkoa wa Iringa ni lazima uwe na mkakati wa kuzipigia debe barabara zote zinazobeba uchumi wan chi kama ilivyo kwa barabara hiyo ya hifadhi ya Ruaha. Tuunde timu na kwa pamoja twendeni serikalini,” alisema Naibu Waziri wa Maliasilia na Utalii, Mahamudu Mgimwa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa, Steven Mhapa alisema ubovu wa barabara hiyo umeendelea kuzorotesha sekta ya utalii katika hifadhi hiyo kubwa kuliko zote nchini.

“Yawezekana kabisa hata hao watalii wachache wanaokuja, hawarudi tena na wala hawana muda ya kusimulia mazuri wanayoyaona katika hifadhi hiyo kwasababu ya ubovu wa barabara hiyo,” alisema.

Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Profesa Peter Msolla alisema mbali na kuikuza sekta ya utalii mkoani Iringa, kujengwa kwa kiwango cha lami kwa barabara hiyo kutachochea uanzishwaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi zenye mahusiano na sekta hiyo na hivyo kusaidia kuongeza ajira hususani kwa vijana.

“Mazingira yakiboreshwa, kampuni za wasafirishaji na waongoza watalii zitaongezeka sambamba na shughuli zingine za kiuchumi kama ujenzi wa migahawa ya kisasa, hoteli na utengenezaji na uuzaji wa bidhaa mbalimbali za kitalii zikiwemo zile za kitamaduni na hivyo kutanua wigo wa ajira na ukuaji wa uchumi nchini,” alisema.

Awali Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoa wa Iringa, Mhandisi Paulo Lyakurwa alisema baada ya Rais Kikwete kutoa ahadi ya kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami mwaka 2010, ziko baadhi ya kazi ambazo tayari zimefanywa.

Alizitaja kazi zilizofanywa kuwa ni pamoja upembuzi yakinifu, tathmini ya athari kwa jamii na mazingira, usanifu wa kina na kuandaa makabrasha ya zabuni.

Lyakurwa alisema katika kuitekeleza ahadi hiyo ya Rais jumla ya kilomita 14.4 toka Iringa Mjini hadi Kalenga zimeshajengwa kwa kiwango cha lami na hivyo kufanya kiasi kilichobaki hadi kufika geti kuu la kuingilia hifadhi hiyo kuwa ni kilomita 90.


Desemba mwaka 2011, Lyakurwa alikiambia kikao hicho kwamba zaidi ya Sh Bilioni 96.4 zinahitajika kwa ajili ya upembuzi, usanifu na ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

Kamati itakayokutana na viongozi hao inajumuisha mkuu wa mkoa, katibu tawala wa mkoa, wakuu wa wilaya, wabunge na meneja wa Tanroads

Reactions:

0 comments:

Post a Comment