Thursday, 8 January 2015

MWENYEKITI WA CHADEMA IRINGA MJINI KUFIKISHWA MAHAKAMANI WAKATI WOWOTE KUANZIA SASA


SIKU 14 alizopewa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa Iringa Mjini, Frank Nyalusi kuitisha mkutano wa hadhara na kukanusha madai ya kutishiwa kuuawa, zimeisha leo na wakati wowote kuanzia sasa atafikishwa mahakamani.

Katika mkutano wa chama hicho, uliofanyika katika viwanja vya Mwembetogwa Desemba 21, mwaka jana, Nyalusi alitoa tuhuma zinazodaiwa kuwa si za kweli na upande unaomlalamikia; zikumuhusisha Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Salim Asas kuwatuma vijana watatu kwenda kumuua.

Asas kwa kupitia wakili wake, Alfred Kingwe alikanusha tuhuma hizo kwa madai kwamba ni za kupikwa na zilitolewa hadharani na Nyalusi kwa lengo la kujiongezea umaarufu.

Ili kumsafisha mteja wake na tuhuma hizo, wakili Kingwe kama alivyoelekezwa na Asas alimkabidhi Nyalusi hati ya madai iliyompa siku 14 kiongozi huyo wa Chadema ambaye pia ni diwani wa kata ya Mivinjeni, awe ameitisha mkutano katika eneo lile lile na kukanusha tuhuma hizo.

Siku 14 baada ya kukabidhiwa hati hiyo ya madai zimeisha jana kwa mujibu wa wakili huyo na hatua inayofuata ni kumfikisha kiongozi huyo wa Chadema mahakamani ili akatoe ushahidi wa madai hayo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment