Friday, 16 January 2015

MKOA WA IRINGA WAPATA KITUO CHA AFYA CHA KWANZA CHA UPASUAJI WAJAWAZITO

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Pudenciana Kisaka akikata utepe kuzindua jengo la upasuaji wajawazito katika kituo cha afya cha Nzihi
Kinavyoonekana kwa mbali
Mandhari yake ya ndani
Sehemu ya kupumzikia wajawazito
Baadhi ya wananchi walioshiriki uzinduzi huo
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Samwel Nkya

KITUO cha Afya cha Nzihi kilichopo kilomita 28 kutoka Iringa mjini kimekuwa cha kwanza kati ya vituo vya afya 22 vya mkoani Iringa kutoa huduma ya dharula ya upasuaji kwa wajawazito.

Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Samwel Oberlin Nkya inaonesha zaidi ya Sh Milioni 160 zimetumika kujenga jengo la upasuaji katika kituo hicho.

Alisema jengo hilo limejengwa kwa ufadhili wa Shirika la Asante Sana lililotoa Sh Milioni 90, nguvu kazi ya wananchi Sh Milioni 12 na mfuko wa pamoja wa wahisani uliotoa Sh Milioni 58.

“Lengo la ujenzi huu ni kuboresha huduma za afya katika kata ya Nzihi na maeneo jirani. Upasuaji mkubwa na mdogo utakaojumuisha upasuaji wa dharula na ule wa kawaida kwa wajawazito utatolewa,” Nkya alisema.

Alisema kabla ya ujenzi huo, wajawazito 35 hadi 50 wamekuwa wakipokelewa na kujifungua kwa njia ya kawaida katika kituo hicho kinachohudumia kaya 4,982 za kata hiyo.

Akizindua huduma ya upasuaji wajawazito wakati wa uzinduzi wa jengo juzi, mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Pudenciana Kisaka alisema; “tunajivunia kuwa wa kwanza katika mkoa wa Iringa kuanza kutoa huduma hii muhimu katika moja ya vituo vyetu vya afya.”

Alisema kukamilika na kuanza kutolewa kwa huduma hiyo katika kituo hicho kutamaliza kero iliyokuwa ikiwasibu wajawazito wa kata ya Nzihi na maeneo jirani na kata hiyo waliokuwa wanalazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo.

Alisema kabla jengo hilo halijakamilika, wajawazito walikuwa wakitegemea kupata huduma hiyo katika hospitali teule ya wilaya ya Iringa ya Tosamaganga na hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa.

Mbali na kupunguza gharama za uendeshaji na matengenezo ya magari ya wagonjwa, Kisaka alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza vifo vya wajawazito vinavyotokana na matatizo ya uzazi yanayohitaji upasuaji wa dharula.

Baada ya kuzindua huduma hiyo, Kisaka na maafisa wengine waliohudhuria uzinduzi huo walipata fursa ya kumshuhudia Erica Ng’engula (27) akijifungua kwa njia ya upasuaji.

Kaimu Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya cha Nzihi, Dk Hans Ngemera alisema ilichukua takribani dakika 50 kukamilisha shughuli hiyo ya upasuaji iliyomuwezesha Ng’engula kupata mtoto mchanga wa kike aliyekuwa na uzito wa kilo 3.4.

Mmoja wa wajawazito aliyekutwa akisubiria kujifungua katika kituo hicho, Blandina Madega alisema ni faraja kwao kuona serikali inazidi kuboresha huduma za afya kwa wajawazito.

“Itatupunguzia wajawazito gharama za kukodi magari ya kutupeleka hospitali ya wilaya na gharama zingine wakati tunasubiri huduma katika hospitali hiyo,” Madega alisema.

 Mmoja wa wazee wa kijiji cha Nzihi, Abiba Ngasi alisema; “sifahamu nitumie lugha gani kuishukuru serikali. Kabla ya jengo hili familia zetu zilikuwa zinalazimika kutumia hadi Sh 60,000 kukodi gari kwa ajili ya kupeleka mjamzito anayehitaji huduma ya dharula katika hospitali ya wilaya au ya mkoa.”

Reactions:

0 comments:

Post a Comment