Sunday, 18 January 2015

MIKOA YA IRINGA NA NJOMBE YAAMSHA MAPAMBANO DHIDI YA LUMBESA

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk Rehema Nchimbi
Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Iringa, Lucas Mwakabungu
Mkuu wa Wilaya ya Wanging'ombe Estalina Kilasi, wa Ludewa Juma Madaha, wa Makete Josephine Matiro na Kilolo Gerald Guninita
Baadhi ya washiriki toka sekta binafsi na umma
Katika majadiliano
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza
MIKOA ya Iringa na Njombe imezinduka kutoka katika kile kilichoitwa na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk Rehema Nchimbi “usingizi dhidi ya vipimo batili vya lumbesa” kwa kuunda kikosi kazi kitakachoamsha na kuchochea mapambano yake.

Kikosi kazi hicho kinachojumuisha wajumbe 10 wa mikoa hiyo kiliundwa juzi, katika mkutano wa wadau kutoka sekta ya umma na binafsi wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa sheria ya mizani na vipimo ya mwaka 1982; uliokuwa uhudhuriwe na waziri wa kilimo chakula na ushirika na waziri wa viwanda na biashara.

Mbali na kushindwa kutuma wawakilishi wao, mawaziri walishindwa kuhudhuria mkutano huo uliofanyika Makambako wilayani Njombe kwa uratibu wa Chemba ya Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoa wa Iringa kupitia mradi wake wa unaofadhiliwa na shirika la BEST AC.

Katibu Mtendaji wa TCCIA mkoa wa Iringa, James Sizya alisema kikosi kazi kilichoundwa na mkutano huo na ambacho kitakutana hivi karibuni kwa ajili ya kupanga utekelezaji wa ufuatilia wa utekelezaji wa sheria hiyo, kinajumuisha maafisa kilimo na biashara, polisi, wakulima na wafanyabiashara wa mikoa hiyo.

Sizya alisema kikosi kazi hicho kinatajiwa kupata msaada wa hali na mali kutoka kwa wakuu wa mikoa na wilaya za mikoa hiyo, makamanda wa Polisi wa mikoa na wilaya, Sumatra, Tanroads, wakurugenzi wa halmashauri na wakala wa mizani na vipimo, wakulima na wafanyabishara.

“Ni kama tumelala katika vita hii inayotishia uhai wa maendeleo ya mkulima. Nakumbuka miaka fulani vita dhidi ya vipimo batili vya mazao ya mkulima ilianza kuleta mafanikio, lakini tukajisahau. Muda wa kuamka umefika,” alisema mkuu wa mkoa wa Njombe.

Akifungua mkutano wa wadau wa hao, Dk Nchimbi alisema kila mahali wanunuzi wamekuwa kiashiria cha kutotekeleza sheria hiyo ambayo lengo lake ni kumkomboa mkulima kutokana na jasho lake la shambani.

“Ipo tabia ya mnunuzi, iwe kwa matumizi yake binafsi au biashara, kuomba nyongeza kwa kila kitu; nyongeza kwa mazao, sukari, chumvi na wakati mwingine hata nyama kwasababu tu ya kutotaka kutumia vipimo halali, hiyo yote ni kuchochea lumbesa” alisema.

Alisema vita dhidi ya lumbesa inatakiwa kuamshwa kwa kasi kubwa itakayokwenda sambamba na utoaji wa elimu kwa watanzania wote ili mafanikio yake yawe ya muda mfupi tofauti na kama ilivyo kwa baadhi ya oparesheni zinazoendelea kutekelezwa nchini.

“Mtakumbuka suala la vizibiti mwendo kwenye mabasi ‘speed governor’ na kampeni ya matumizi ya kondomu. Nyinyi wenye ni mashahidi yapo mabasi yanayokwenda kwa mwendo unaoashiria kwamba hayana vidhibiti mwendo na katika baadhi ya maeneo tuangalie jinsi maambukizi ya VVU yanavyoongezeka, hiyo ni kuashiria kwamba kondomu hazitumiki,” alisema.

Mwenyekiti wa TCCIA wa mkoa wa Iringa, Lucas Mwakabungu alisema katika mkutano huo kwamba wakati mikoa hiyo ikielekea kuamsha mapambano dhidi ya Lumbesa, bunge kwa upande wake linatakiwa kuifanyia marekebisho sheria ya mizani ya vipimo ya mwaka 1982 kwa kuwa mswada wake wa marekebisho upo tayari.

“Muswada wa marekebisho ya sheria hiyo uliandaliwa mwaka 2013 (the weight and measures bill, 2013). Katika muswada huo inapendekezwa adhabu na faini kwa asiyefuata sheria iongezwe” alisema na kuongeza kwamba faini kwa kosa hilo kwasasa ni Sh 100,000.

Alisema utafiti wao kuhusu vipimo vya Lumbesa unaonesha serikali imekuwa ikipoteza zaidi ya Sh Bilioni 14.8 kama mapato ya kodi huku wakulima nchini kote wakipata hasara ya zaidi ya Sh Bilioni 174 kila mwaka.


“Na kwa mikoa ya Iringa Njombe, serikali imekuwa ikipoteza zaidi ya Sh bilioni 2.5 kila mwaka huku wakulima wakipoteza zaidi ya Sh bilioni 14.7,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment