Monday, 5 January 2015

KUNDI LA WHATSAPP LATOA MSAADA MKUBWA KWA WATOTO YATIMA WA IMAGE, KILOLO

Baadhi ya members wa kundi hilo wakihakiki bidhaa walizopeleka kwa watoto hao
Frank Leonard (kushoto) na Denis Mlowe (kulia) wakikabidhi sehemu ya msaada wao kwa mratibu wa kituo hicho, Dk Fausta Chota
Anita Boma kushoto naye akasaidia kukabidhi msaada huo
Clement Sanga (mwenye miwani) pamoja na Janeti Matondo wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watoto wa kituo hicho
Katika picha ya pamoja na watoto hao
Oliva Motto na watoto hao
Denis Mlowe na watoto hao

Jamaa wakisaidia kuingiza ndani msaada wetu katika kituo hicho
Ziada na Denis wakigawa maziwa kwa baadhi ya watoto hao
WATU 100 wanaounda mtandao wa simu za mkononi wa Bongo Leaks Whatsapp, wameonesha namna mitandao ya kijamii inavyoweza kuhamasisha maendeleo baada ya kuchangishana fedha na kusaidia kituo cha Image Namba Mbili kinacholea watoto yatima wakiwemo wale wenye ulemavu.

Kituo hicho kilichopo tarafa ya Mazombe, wilayani Kilolo mkoani Iringa kinajulikana kwa jina la kituo cha watoto yatima na walemavu cha Mtakatifu Felix kilichoanzishwa na Padri Phillipo Mammno kutoka Italia.

Zaidi ya Sh 500, 000 zilizochangwa na wanachama wa mtandao huo ulioasisiwa na mwanahabari Frank Leonard wa mjini Iringa ziliwawezesha watoto hao zaidi ya 110 kupata sukari kilo 50 na ngano kilo 50.

Vingine vilivyotolewa kwa watoto hao ni pamoja na mafuta ya kula lita 50, sabuni za kufulia roba mbili, mchele kilo 40, juice na biskuti.

Katika kuunga mkono kilichofanywa na kundi hilo, kampuni ya maziwa ya Asas Dairies ltd ilichangia pakti 200 za maziwa aina ya mtindi huku mwanahabari wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) mkoani Iringa, Irine Mwakalinga akitoa msaada wa nguo kwa baadhi ya watoto hao.

Mratibu wa kituo hicho, Dk Fausta Chota alisema kwa wastani kituo kinatumia zaidi ya Sh 500,000 kwa mwezi kwa mahitaji ya kawaida ya watoto hao.

“Kiasi hicho ambacho ni nje ya gharama zingine kama za mavazi, matibabu, sabuni na mafuta ni kwa ajili ya chai na chakula cha mchana na jioni kwa watoto hao,” alisema.

Alisema sehemu kubwa ya gharama hiyo inatolewa na Padri Mammno ambaye kwa muda mrefu amekuwa akikiri kuelemewa na mzigo huo hali inayokiweka kituo hicho katika mazingira ya kushindwa kuwapokea watoto wengi zaidi.

Padri Mammno amenukuliwa mara kwa mara na vyombo mbalimbali vya habari akiiomba serikali isaidie gharama za kuhudumia kundi hilo la jamii.

Mbunge wa jimbo la Kilolo, Profesa Peter Msolla alipoulizwa kuhusiana na mchango wa serikali katika kituo hicho alisema; “kwa maelezo ya Padri Mammno inaonekana tangu kianzishwe hakijawahi kupokea msaada wowote toka serikalini.”

Alisema atakutana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo ili kujua ni kwanini kituo hicho hakipelekewi msaada wowote toka serikalini.

Kwa mujibu wa Dk Chota, kati ya watoto yatima 111 wanaolelewa katika kituo hicho, 93 ni walemavu wa viungo huku baadhi yao wakiwa na mtindio wa ubongo.

Dk Chota alisema kituo hicho kinaweza kusitisha huduma kwa watoto hao kama kwa mazingira yoyote yale huduma ya Padri Mammno itakoma.

Mmoja wa walemavu anayelelewa katika kituo hicho toka mwaka 1993, Charles Kiwele alisema maisha yake yamenusurika toka apelekwe na ndugu zake katika kituo hicho.

“Toka waliponileta mwaka 1993, hawajawahi kumtembelea kituoni hapo. Sijui walipo na sijui kinachoendelea lakini napenda wajue kwamba mimi mwenyewe naendelea vizuri,” alisema.

Kwa uchungu aliwatakia kila la kheri katika maisha yao na kumuomba Mwenyezi Mungu awape maisha marefu na afya njema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment