Tuesday, 13 January 2015

KINGUNGE ANENA-MATUMIZI YA FEDHA YANAYOFANYWA NA WANA CCM SIO HOJA


MWANASIASA mkongwe nchini, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru, ameshangazwa na baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kulalamikia matumizi makubwa ya fedha kwa baadhi ya wanachama wake ndani ya chama hicho.

Alisema suala hilo halipaswi kuwa ajenda ndani ya chama bali kinachotakiwa ni kuangalia namna ya kushughulika nalo kwani suala hilo limekuwepo miaka mingi ndani, nje ya nchi.

Mzee Kingunge aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza kwenye kituo kimoja cha redio na kusisitiza kuwa, fedha zimekuwa zikitumika ili kuuza haki, wengine wakitaka kupata upendeleo jambo ambalo halikufanyika katika uongozi wa Awamu ya Kwanza pekee bali limeanzia katika utawala wa kikoloni.

“Nashangaa kuona suala hili linaibuka sasa likiambatana na maneno kama rushwa, mlungula na hongo, biongozi nao wanalazimisha kuliondoa katika jamii.

“Sisi tulikuwa tukipiga vita mwanzoni kwa uhuru tukiwaeleza wanachama kwamba, matukio haya hayakuwa jambo la kawaida katika vyama vya TANU, Afro Shirazi Party (ASP) na CCM,” alisema Mzee Kingunge.

Akizungumzia Miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar, alisema viongozi wanapaswa kuyaenzi kwa vitendo kwani katika Bara la Afrika ni tukio kubwa ambalo waasisi wake waliwaonesha wakoloni kuwa hawataki kudharauliwa wala kunyanyaswa.

Alisema kila mwaka, Wazanzibari wamekuwa na utaratibu wa kuyaenzi Mapinduzi hayo kwa vitendo ambapo kamati ya watu 14 iliyokuwa chini ya Seif Bakari, iliweza kufanya mambo yote ya kuhakikisha kuwa Mapinduzi yanapatikana.

“Lengo lilikuwa ni kurejesha utu wao na ndio maana wakadai nchi yao ili waweze kupata madaraka ya kisiasa ambayo yaliweza kukomesha unyonge wa kunyanyaswa kwa Mwafrika.

“Kuwaenzi waasisi wa Mapinduzi kwa kufanya kumbukumbu ya mara moja kwa mwaka haitoshi bali tunapaswa kuendeleza zaidi ili kuonyesha siku hiyo ni muhimu,” alisema.

Akitolea mfano wa Desemba 9 ambayo Tanzania Bara ilipata uhuru wake, Mzee Kingunge alisema kuwa kuwa siku hiyo ni muhimu inayopaswa kuendelezwa kwa vitendo.

Alisema harakati za mapambano ya kupigania uhuru katika baadhi ya nchi kama Tanzania Bara, Zanzibar, Kenya, Uganda, Congo na nyinginezo zilikuwa na lengo moja la kukomesha vitendo vya unyanyasaji, umaskini na maradhi.

Mzee Kingunge alisema; “Tunapaswa kujiuliza kuwa harakati za waasisi wetu waliopigania uhuru tumewasahau...lazima tukumbuke walikuwa wanapigania nini.

“Suala la kumkomboa Mwafrika linasuasua, vipaumbele vya nchi haviendani na malengo ya kujenga utu wa Mwafrika na heshima yake duniani,” alisema.

Januari 3, mwaka huu, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Bw. January Makamba katika Sherehe za Maulidi ya Kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W), iliyofanyika Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, aliwataka Watanzania kuwaepuka viongozi wanaotafuta uongozi kwa fedha nyingi kwani wakifanikiwa kuingia madarakani hawataweza kutawala kwa haki.

Mbali na Makamba pia makada kadhaa wa CCM akiwemo Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara na Waziri Mkuu mstaafu, Bw. Frederick Sumaye, kwa nyakati tofauri wamekuwa wakilia na rushwa bila kutaja jina la nani anayehusika na vitendo hivyo.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe, alilalamikia vitendo vya rushwa na kudai kundi la mafisadi wamekuwa wakimchukia.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment