Thursday, 15 January 2015

KESI YA MAUAJI YA MWANGOSI KUUNGURUMA KWA WIKI NZIMA MAHAKAMA KUU KANDA YA IRINGA


KESI ya mauaji ya aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa Channel Ten Mkoani Iringa na Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC), Daudi Mwangosi itaendelea kusikilizwa Februari 12 hadi 18, mwaka huu.

Kesi hiyo inayomkabili aliyekuwa askari wa jeshi la Polisi, Pacificius Cleophace Simoni itaendelea kusikilizwa mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mary Shangali baada ya upande wa mashtaka kuileza mahakama hiyo kwamba uchunguzi wake umakamilika.

Jaji Shangali aliahidi kuwaruhusu wanahabari kushiriki kikamilifu katika kesi hiyo ikiwa ni pamoja na kupiga picha kabla shughuli za mahakama hiyo hazijaanza.

Uamuzi huo wa Jaji unalenga kumaliza kitu kinachoonekana kama ghasia zisizo na maana wanazofanyiwa wanahabari wakati mtuhumiwa huyo anapofikishwa mahakamani.

Mbali na kufikishwa mahakamani hapo akiwa katika magari tofauti na yale yanayotumika kubeba watuhumiwa wengine, baadhi ya Polisi wanaofuatilia kesi hiyo wamekuwa wakimzingira mtuhumiwa huyo ambaye mara zote amekuwa akivaa vazi linaloficha sura yake na wakati huo huo wamekuwa wakiwafukuza na kuwazuia wanahabari kupiga picha za mtuhumiwa huyo.

Wakati ikisikilizwa kwa mara ya kwanza Februari 13, mwaka jana, Wakili wa upande wa mashtka, Adolph Maganga alisema, kwa kukusudia mtuhumiwa Pacificius Cleophace Simoni anatuhumiwa kumuua Mwangosi kinyume na kifungu cha sheria ya kanuni ya adhabu namba 196 sura ya 16 kilichofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Alisema katika tukio hilo lililotokea Septemba 2, 2012 katika kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi mkoani Iringa, mshtakiwa alifyatua bunduki yake na kusababisha kifo cha marehemu, papo hapo.

Alisema siku ya tukio marehemu alikuwa Nyororo kwa ajili ya kuripoti na kutoa taarifa kwa umma juu ya mkutano uliokuwa ufanywe na katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Wilbroad Slaa.

Alisema mshtakiwa akiwa mmoja wa wafanyakazi wa Polisi, waliwasihi Chadema wasifanye mkutano huo kabla wafuasi wake hawajaanza kurusha mawe kwa Polisi na baadhi yao kupata majeraha.

Kutokana na mzozo huo, wakili huyo wa serikali alisema polisi walipiga mabomu ya machozi ili kuwatawanya wafuasi hao kabla mshtakiwa huyo hajamfyatulia bomu marehemu.

Wakili huyo aliwasilisha ramani ya eneo la tukio, ripoti ya mtaalamu wa milipuko na ripoti ya daktari aliyechunguza mwili wa marehemu Mwangosi na gazeti la Mwananchi la Septemba 3, 2012 lililochapisha  picha ya tukio hilo katika ukurasa wa mbele kama vielelezo vinavyohusiana na kesi hiyo.

Wakili wa upande wa utetezi Lwezaula Kaijage alitaja mambo wanayokubaliana katika kesi hiyo kuwa ni jina na anuani ya mshtakiwa na kwamba marehemu Mwangosi alikufa kifo ambacho si cha kawaida.

Na kwamba mshtakiwa Simoni alikamatwa na amefikishwa mahakamani akihusishwa na mauaji hayo.

Wakili Kaijage alisema vielelezo vingine vilivyoletwa na upande wa mashtaka hawakubaliani navyo kwakuwa vinahitaji ushahidi kutoka kwa wahusika.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment