Monday, 19 January 2015

FLIGHT LINK YALETA NDEGE KUBWA IRINGA, KUTUA MARA TANO KWA WIKI

Mkurugenzi wa Masoko wa Flight Link, Ibrahim Bukenya na Afisa Masoko wa kampuni hiyo mkoani Iringa, Imani Robert
Wakizungumza na baadhi ya wanahabari wa mjini Iringa
NDEGE za shirika la ndege la Flight Link zitaanza kutua mara tano kwa wiki katika uwanja wa ndege wa Iringa (Nduli) ikiwa ni matokeo ya jitihada zake za kukidhi mahitaji ya ongezeko la abiria wanaotumia uwanja huo.

Hatua hiyo imekuja wiki mbili tu baada ya Waziri wa Uchukuzi, Dk Harison Mwakyembe kutembelea uwanja huo na kuahidi kuzishawishi kampuni za ndege zinazochukua abiria wengi zaidi kutoa huduma hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Thomas Haule wakati wa ziara ya waziri huyo inaonesha kuwepo kwa ongezeko kubwa la abiria wanaotumia uwanja huo.

Haule alisema wakati mwaka 2009 kulikuwa na abiria 756 waliotumia uwanja huo kupitia ndege za kukodisha na zile za ratiba maalumu, mwaka 2012 na 2013 waliongezeka hadi kufikia 9,213 na 9,808.

Alisema abiria walitarajiwa kuongezeka zaidi mwaka 2014 lakini walipungua hadi 7,226 kutokana na udogo na uchache wa ndege zinazofanya safari za ratiba maalumu na za kukodisha.

Akizungumza na wanahabari jana, Mkurugenzi wa Masoko wa Flight Link, Ibrahim Bukenya alisema ndege zao zitaanza kutoa huduma hiyo mara tano kwa wiki zikitokea jijini Dar es Salaam.

“Kuanzia tarehe 26 mwezi huu wa kwanza tunaanza kutoa huduma hiyo. Safari zetu zitakuwa zinaanzia Dar es Saam kupitia Dodoma n kuja Iringa na kisha kurudi Dar es Salaam,” alisema.

Alisema safari hizo zitakuwa kila jumatatu, jumanne, jumatano, alhamisi na ijumaa huku mipango yao ya baadaye ikiwa ni kuongeza ili ziwe za kila siku.

“Habari njema kwa watu wa Iringa ni kwamba tunaleta ndege kubwa itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 30. Ndege hiyo ina ingini mbili na inatumia dakika 50 hadi saa moja kutoka Iringa hadi Dar es Salaam,” alisema.

Bukenya alisema kuanzishwa kwa safari hiyo kutawawezesha wananchi wakiwemo wafanyabiashara kutumia muda mfupi katika safari na kuongeza tija katika shughuli zao na kuchochea shughuli za utalii mkoani Iringa.

Kuhusu huduma kwa mteja, alisema mbali na huduma mbalimbali za kuvutia atakazokuwa akipewa mteja ndani ya ndege zao, kuna fursa ya bure ya kusafirisha kilo 20 za mzigo na kilo tano zingine za mzigo ambao abiria anaweza kuingia nao ndani ya ndege.


Bukenya alisema wakati likiingia mkoani Iringa shirika lao linaendelea kutoa huduma za safari katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Dar es Salaam,  Arusha, Serengeti, Selou, Zanzibar, Pemba na Dodoma.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment