Wednesday, 7 January 2015

DOKTA MWAKYEMBE AHOFU CCM KUPOTEZA VITI VINGI UCHAGUZI MKUU WA MWAKA HUU


WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harison Mwakyembe ameuzungumzia Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu akisema ana hofu Chama cha Mapinduzi (CCM) kitapoteza nafasi nyingi za uongozi kama wataendelea kusigana wenyewe kwa wenyewe.

Katika uchaguzi huo aliosema utakuwa mgumu kutokana na mazingira ya kisiasa yalivyo hivisasa, madiwani, wabunge na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar wanatarajia kuchaguliwa.

“Ushindi kwa wenzetu utakuwa mkubwa sana kama CCM tusipotambua hilo, tukiendelea kuchapana makonde sisi wenyewe tutawapa wenzentu nafasi ya kupita,” alisema bila kutoa ufafanuzi wa misigano hiyo.

Akizungumza na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa mara baada ya kukagua kiwanja cha ndege cha mjini Iringa katika ziara yake ya siku moja ya mjini hapa, Dk Mwakyembe alisema; “halitakuwa jambo la kufurahisha ikiwa hilo litatokea.”

Katika ziara hiyo, waziri huyo alipata fursa pia ya kuzungumza na wadau wa sekta ya usafirishaji wa mkoa wa Iringa waliompa kero mbalimbali zinazowakabili katika kutoa huduma hiyo.

Alisema kazi iliyofanywa katika kukijenga chama hicho na imani waliyonayo watanzania juu yake haipaswi kuachwa iteketete kwasababu ya tofauti ya wachache.

Kauli ya Dk Mwakyembe inarejea makundi ya kisiasa yanayozidi kuibuka ndani ya chama hicho kwasababu ya kutafuta nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo.

Makundi hayo yanahusu wagombea wa urais, ubunge na udiwani ambayo kama hayatavunjika baada ya kura za maoni za chama hicho, kwa mujibu wa Dk Mwakyembe yatakidharirisha chama hicho.

Akitoa mfano wa jinsi CCM ilivyoimarishwa kwa mika mingi, alisema CCM haipaswi kufafanishwa na mpishi aliyepika maharage yake kwa muda mrefu na yanapokaribia kuiva anaanza kubishana kuhusu nani apewe kijiko ili ayale.

Ubishi huo unaokwenda sambamba na kupakana matope, unaweza kutoa fursa kwa mujibu wa waziri huyo, kwa asiyehusika kuyala maharage hayo yote.

Pamoja na kwamba Dk Mwakyemba hajatangaza nia ya kuwania nafasi ya urais wan chi, baadhi ya wana CCM waliohojiwa juu ya mtazamo wao dhidi ya waziri huyo, kwa sharti la kutotaja majina yao walisema kama ataingia katika kinyang’anyiro hicho basi anafaa kuwa mgombea urais kupitia CCM.

“La kwanza kabisa nalofahamu kuhusu Dk Mwakyembe ni kwamba hana kashfa, tofauti na wanasiasa wengine wanaotajwa ndani na nje ya CCM,” alisema mmoja wao.

Alisema sifa nyingine ambazo zinampambanua Dk Mwakyembe ni uadilifu alionao katika kusimamia kazi zinazotekelezwa chini ya mamlaka yake.

Tofauti na vyama vingine vya siasa, wagombea wengi waliotangaza nia na wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ya juu kabisa ya nchi ni wale wanaotoka CCM.

Walionukuliwa kutanganza nia ni pamoja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, Mbunge wa Nzega Dk Hamis Kigwangalla, Waziri wa Maliasilia na Utalii Lazaro Nyalandu na Waziri Mkuu Mizengo Pinda anayedai kutangaza nia hiyo kimyakimya.

Wengine wanaotajwatajwa kuutaka urais kupitia chama hicho ambao hata hivyo hawajatangaza rasmi nia hiyo ni pamoja na mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.

Wapo pia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Waziri wa Katiba na Sheria Dk Asha Rose Migoro.

Wengine ni pamoja na mbunge wa Sengerema William Ngeleja na mbunge wa Songea Mjini Dk Emanuel Nchimbi ambao kwa pamoja wamewahi kuwashika nafasi za uwaziri katika serikali ya awamu ya nne, kabla ya uteuzi wao kutenguliwa.

Wakati Ngeleja aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Nishati na madini kabla ya kupandishwa na kuwa waziri kamili wa wizara hiyo, Dk Nchimbi naye aliwahi kuwa naibu waziri wa mambo ya ndani kabla hajateuliwa kuwa waziri kamili wa wizara hiyo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment