Sunday, 4 January 2015

DC GUNINITA AMPIGIA DEBE PROFESA PETER MSOLLA UBUNGE WA KILOLO 2015

Dc Gerald Guninita
Mbunge wa Kilolo, Profesa Msolla
MKUU wa wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Gerald Guninita amempigia chapuo  mbunge wa sasa wa jimbo la Kilolo, Profesa Peter Msolla akisema “kwa kazi kubwa anazofanya” anastahili kuchaguliwa kwa mara nyingine tena kuwa mbunge wa jimbo hilo, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

“Nimeguswa na namna Profesa Msolla alivyotekeleza na anavyoendelea kutekeleza ahadi alizozitoa katika uchaguzi mkuu wa 2010 na jinsi anavyoshirikiana vyema na serikali ya Chama cha Mapinduzi kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2010,” alisema.

Alisema sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo ya elimu, afya, barabara, mawasiliano, kilimo, biashara, usafirishaji na nyingine nyinngi zimepiga hatua kubwa jimboni humo kutokana na mchango mkubwa wa mbunge huyo.

“Na kubwa lililofanywa hivi karibuni ni la kuidhinisha zaidi ya Sh Milioni 52 za mfuko wa jimbo zitumike kusaidia ujenzi wa maabara na maendeleo ya sekta ya elimu jimbo humo huku yeye mwenye akichangia kutoka mfukoni mwaka Sh milioni moja,” alisema.

Aliyasema hayo kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) ya Kilolo kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, mjini Kilolo baada ya Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Iringa, Oscar Ndale kuwasilisha ombi la kugawa jimbo hilo katika kikao hicho.

“Mheshimiwa mwenyekiti wa kikao hiki muhimu cha DCC, Chadema tunaleta ombi maalumu la kuligawa jimbo hili kutokana na jiografia yake ilivyo,” Ndale ambaye pia ni mjumbe wa kamati tendaji ya Chadema ya Kilolo alisema.

Alisema pamoja na ukubwa wa wilaya hiyo, Ndale alisema imeendelea kuwa na jimbo moja tofauti na wilaya ya Iringa yenye majimbo matatu; Iringa Mjini, Isimani na Kalenga na Mufindi yenye majimbo mawili ya Mufundi Kaskazini na Mufindi Kusini.

Akitangaza kiaina kugombea ubunge katika jimbo hilo, Ndale alisema kwa ukubwa wake, wilaya hiyo inapaswa kuwa na majimbo mawili, moja akiliita la Ilula hasa baada ya mji wa Ilula kupata hadhi hivikaribuni na kuwa na halmashauri ya mji mdogo inayohusisha tarafa ya Mazombe na Ruaha Mbuyuni na jimbo lingine alilosema liitwe jimbo la Kilolo, linalohusisha tarafa ya Kilolo.

“Binafsi kama jimbo hili litagawanya na kuwa na majimbo ya Ilula na Kilolo, mimi nitagombea jimbo la Kilolo na Profesa Msolla tutamuachia agombee jimbo la Ilula ambako ni ukanda anakotokea” alisema katibu huyo wa Chadema.

Katika majibu yake kwa kiongozi huyo wa Chadema, Profesa Msolla alikiri jimbo hilo kuwa kubwa kuliko jimbo lingine lolote mkoani Iringa, lakini linalokosa vigezo vya kugawanywa kwa sasa.

Alivitaja baadhi ya vigezo vinavyotumiwa na tume ya Taifa ya Uchaguzi kugawa majimbo kuwa ni pamoja na mipaka ya kiutawala, mgawanyo wa wastani wa idadi ya watu, mawasiliano, jiografia na hali ya uchumi.  

Katika mkutano huo wa DC, Profesa Msolla alimshukuru mkuu huyo wa wilaya kwa kumtakia kila la kheri katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu na akasisitiza nia yake ya kuwania tena nafasi hiyo ya ubunge ili akamilishe ndoto za kimaendeleo alizonazo kwa watu wa jimbo hilo.

“Pamoja na kazi nyingine nyingi, moja ya kazi kubwa iliyoko mbele yangu ni kuhakikisha barabara ya Iringa hadi Kilolo inajengwa kwa kiwango cha lami, na kuhakikisha tatizo la maji katika mji wa Ilula ambalo linatokana na ongezeko kubwa la watu linamalizwa katika kipindi kifupi kijacho,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment