Wednesday, 28 January 2015

BALOZI WA JUMUIYA YA ULAYA NA NAIBU WAZIRI WA AFYA WAZINDUA MRADI WA USAFI IRINGA


Balozi wa EU, Filiberto Ceriani Sebregondi ( wa pili kulia), Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza (wa kwanza kulia), Naibu Waziri wa Afya, Dk Steven Kebwe na Meneja Mradi wa Usafi Iringa,Joerg Henkel wakiwa wameshika mikataba ya mradi huo wakati wa uzinduzi wake hii leo 

Joerg Henkel akitoa maelezo ya mradi katika moja ya banda la maonesho
Baadhi ya wageni walioshiriki uzinduzi wa mradi huo
Kulikuwa na kundi kubwa la wanafunzi waliofurahia ujio wa mradi huo
waalikwa wengine wakifuatilia yaliyokuwa yakiendelea
BALOZI wa Jumuiya ya Ulaya Nchini, Filibero Ceriani Sebregondi leo amezindua mradi wa usafi wa mazingira na usambazaji wa huduma ya maji mjini Iringa huku Naibu Waziri wa Afya, Dk Kebwe Kebwe akipongeza utekelezaji wake kwamba umezingatia Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mradi huo utakaogharimu zaidi ya Sh Bilioni 2.2 unaratibiwa na asasi ya ACRA-CCS kwa ufadhili wa jumuiya hiyo, unahusisha kata nne za majaribio za Nduli, Kihesa, Mtwivilla na Mkimbizi zilizoko pembezoni mwa manispaa ya Iringa.

Meneja wa mradi huo Joerg Henkel alisema; “lengo la mradi huu uliopewa jina la Iringa Usafi ni kuimarisha afya na hali ya usafi katika maeneo hayo ya pembezoni kwa kuangalia zaidi masuala ya mazingira na uendelevu wa kijamii na kiuchumi.”

Alisema mradi huo miaka mitano ulioanza kutekelezwa Machi 2014 unashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo halmashauri ya manispaa ya Iringa, Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Iringa (IRUWASA), asasi ya Maji na Maendeleo (DODOMA), shirika la IDYDC, CUAM, CEWAS (Uswis), BOKU (Australia) na CeTAmb (Italia).

“Katika kipindi hicho mradi utatambua mifumo ya usafi wa mazingira, utaimarisha mnyororo wa utoaji wa huduma za usafi wa mazingira, utasaidia kubadili tabia katika jamii na kuongeza upatikanaji wa huduma za usafi wa mazingira na maji,” Henkel alisema.

Alisema huduma ya maji na usafi wa mazingira utahusisha ujengaji wa vyoo bora vitakavyomaliza tatizo la baadhi ya watu kujisaidia mahali popote pasipo na huduma hiyo.

“Mradi unatarajia kuwafikia watu 53,000 wanaounda kaya 11,000 ambao ni sawa na asilimia 37.8 ya wakazi wote wa manispaa ya Iringa, na utalenga shule za msingi 48 zenye wanafunzi 40,000 na vituo vya afya na usafi 25” alisema.

Alisema maeneo hayo yatapatiwa elimu ya afya na usafi wa mazingira, kujengewa vyoo na vituo bora vya usafi wa mazingira na kuwekewa vifaa vya kunawia mikono kwa kuzingatia usawa wa kijinsia na makundi ya jamii yenye mahitaji maalumu.

Akizindua mradi huo, Sebrogondi alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, EU iliahidi kutoa Euro 150 milioni kwa ajili ya kugharamia sekta ya maji nchini, kuboresha upatikanaji wa maji safi na usafi wa mazingira mijini na vijijini.

“Lengo letu ni kuisaidia Tanzania hadi mwaka huu utakapokwisha iwe imefikia lengo la millenia namba saba linalohusu huduma ya maji na usafi wa mazingira,” alisema.

Akishukuru kwa msaada huo, Naibu Waziri wa Afya, Dk Kebwe alisema mradi huo utasaidia kupunguza umasikini na kuimariha hali na ubora wa maisha ya wananchi wa mkoa wa Iringa kama malengo ya MKUKUTA 11 yanavyotaka.

“Mradi huo umekuja huku takwimu zikionesha asilimia 12 ya kaya zote nchini ndizo zenye vyoo bora; na wananchi wachache ndio wanapata huduma za maji kwa umbali wa mita 400 na kwamba elimu ya unawaji mikono kwa sabuni katika nyakati muhimu za uzingatiaji wa usafi wa mazingira bado ni duni,” alisema.

Alisema matarajio ya serikali ni kuona mradi huo unaongeza chachu katika ufanisi wa malengo ya utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira kwa kuongeza ujenzi wa vyoo bora katika ngazi ya kaya, shule, vituo vya tiba na maeneo ya barabarani kwa ajili ya wasafiri.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment