Wednesday, 28 January 2015

BAADHI YA WAFANYABIASHARA IRINGA WAFUNGA MADUKA KUSHINIKIZA MWENYEKITI WAO AACHIWE HURU


WAFANYABISHARA wa mjini Iringa, wengi wao wakiwa ni wale wa biashara za madukani wameingia katika siku ya kwanza ya mgomo wao wakipinga kukamatwa na Polisi kwa kiongozi wao wa Kitaifa Johnson Minja.

Taarifa ya vikaratasi ambayo haikusainiwa na mtu yoyote lakini ikihitimisha kwa maneno “kwa pamoja tunaweza” ilisambazwa kwa wafanyabiashara hao juzi.

Kwa kupitia vikaratasi hivyo, wafanyabishara hao walisema; kesho (yaani jana) hatutafungua maduka nchi nzima kwasababu ya kumatwa kwa kiongozi wetu huyo.

Taarifa hiyo ilisema kiongozi huyo alikamatwa katika mazingira ya kutatanisha jijini Dar es Salaam na mpaka sasa hajulikani alipo.

Wakionekana kutekeleza kile kilichoandikwa katika vikaratasi hivyo, jana wafanyabiashara wa maduka mengi ya katikati ya mji wa Iringa yalikuwa yamefungwa kutwa nzima na kusababisha usumbufu mkubwa kwa baadhi ya watu waliokuwa wakihitaji mahitaji.

Mgomo huo umeelezwa kuathiri pia baadhi ya maeneo ya wilaya za Kilolo, Iringa Vijijini na Mufindi.

Pamoja na wafanyabishara wengi wa kati kuitia mgomo huo, baadhi ya wafanyabiashara wa pembezoni mwa mji wa Iringa yakiwemo maeneo ya Nduli, Mtwivilla, Kihesa, Igumbiro, Mkwawa na Mwangata waliendelea na biashara zao kama kawaida.

Mmoja wa wafanyabiashara hao ambaye hata hivyo hakutaka kutaja jina lake kwa hofu kwamba watashughulikiwa na wenzeke wanaoendelea na mgomo huo alisema; “haya mambo yanaendeshwa kisiasa sana na kutuathiri baadhi yetu hasa wenye mitaji midogo inayotokana na mikopo midogo midogo inayohitaji marejesho ya kila wiki.”

Pamoja na kukamatwa kwa kiongozi wao huyo wa kitaifa, kinachogomewa na wafanyabiashara hao ni matumizi ya mashine za kodi (EFD).

“Wagome wanaostahili kutumia mashine hizo, kwanini hata wale wasiostahili kuzitumia nao wanalazimishwa kugoma?.. hii sio haki kabisa,” alisema.

Akizungumzia usumbufu wanaopata wananchi wanaohitaji huduma katika maduka hayo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza alisema; “nimeshindwa kukutana na viongozi wa wafanyabishara wa mkoa wa Iringa hii leo, lakini taratibu zinaendelea kufanywa ili nikutane nao kesho Alhamisi.”

Viongozi wa wafanyabiashara hao wa maduka hawakuweza kupatikana mara moja kuzungumzia hatma ya mgomo huo japokuwa katika vikaratasi vilivyosambazwa wameahidi kuendelea nao mpaka pale kiongozi wao atakapoachiwa huru bila masharti yoyote.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment