Thursday, 25 December 2014

WATENDAJI WA KATA ZA MANISPAA YA IRINGA WAWAPOKEA WASAIDIZI WA KISHERIA WA MAENEO YAO

Katika picha ya pamoja, wasaidizi wa kisheria, maafisa wa kituo cha msaada wa sheria Iringa na watendaji wa kata wakati wa hafla ya makabidhiano ya wasaidizi wa kisheria hao mjini Iringa
Wasaidizi wa kisheria katika picha ya ya pamoja
Watendaji wa kata katika picha ya pamoja
MAAFISA watendaji wa kata 16 za manispaa ya Iringa wamewapokea wasaidizi wa kisheria katika kata zao watakaosaidia jamii, hasa ya watu wasio na uwezo kupata ushauri wa mambo mbalimbali yanayohusu sheria bila malipo yoyote.

Wasaidizi hao wa kisheria wanatarajia kuanza kazi hiyo mapema mwezi Januari, 2015 baada ya Kituo cha Msaada wa Kisheria Iringa (Iringa Paralegal Centre) kuwapa mafunzo.

Mafunzo hayo ya siku tano kuhusu sheria mbalimbali zinazoweza kuwasaidia wananchi kupata haki zao msingi yalifanyika kwa ufadhili wa asasi ya Legela Services Facility ya Denmark.

Kaimu mwenyekiti wa maafisa watendaji wa kata hizo, Wilbert Chahe alishukuru waliobuni mpango huo akisema utawasaidia wananchi wengi, hasa wale wasio na uwezo, kudai, kutetea na kupata haki zao.

“Tunawakaribisha wasaidizi hawa kwa mikono miwili katika kata zetu, wamekuja katika kipindi muafaka ambacho sisi kama watendaji tunaona watasaidia sana kutoa ushauri kwa wana ndoa na mambo mbalimbali yanayohusu urithi, ardhi na haki zingine,” alisema.  

Mratibu wa Kituo cha Msaada wa Kisheria Iringa, Sidified Mapunda; “tunawakabidhi wasaidizi hawa kisheria na mjue kwamba kazi hii wataifanya bure, hawaruhusiwi kuweka tozo la aina yoyote wanapotimiza majukumu haya. Wamekubali kujitolea hivyo wanatakiwa kuifanya kazi hiyo kwa msingi huo.”

Aliyataja majukumu ya wasaidizi wa kisheria kuwa ni pamoja na kutoa msaada wa kisheria, kuelimisha jamii haki zao kisheria na kuelekeza jamii juu ya vyombo mbalimbali vya kupata haki kama Polisi, mahakama na mabaraza ya usuluhishi ya kata.

Zingine ni pamoja na kusaidia kutatua migogoro katika jamii ambayo sio lazima ipelekwe kwenye vyombo vya dola na kuwaandalia wateja hati au nyaraka za kisheria pale inapowezekana.

 “Wito wangu kwa wasaidizi hawa, msitumie lugha za ulaghai kwa wateja wenu, ikiwa ni pamoja na kujiita wanasheria au mawakili na kuanza kutoza gharama za ushauri kama wanavyofanya mawakili,” alisema.
  
Alisema ili wakuwajengea zaidia uelewa wa masuala ya kisheria, wasaidizi hao wa kisheria wataendelea kupatiwa mafunzo ya mara kwa mara katika kipindi cha miaka miwili na nusu.

Wakiyazungumzia mafanikio ya kazi waliyopewa, wasaidizi wa kisheria hao walisema ipo hapa kwa wadau wa mpango huo kuangalia uwezekano wa kuwalipa posho ya kila mwezi.

Katika mapendekezo ya kiasi gani wasaidizi wa kisheria walipwe kama motisha, mmoja wao aliyejitambulisha kwa jina la Jackson Haule alisema; “kwa mazingira ya sasa posho ya Sh 150,000 inaweza kutusaidia kuongeza ufanisi wa kazi hiyo.”

Alisema dhana ya kujitolea ina mipaka yake kwani wanafahamu kuwepo kwa gharama watakazolazimika kuzitumia ili kuifanikisha kazi hiyo.

“Gharama hizo zinahusisha kusafiri kutoka eneo moja hadi jingine, kuchapisha nyaraka mbalimbali, gharama za mawasiliano na zinginezo na kama tukishindwa na wateja wetu wakatugharamia dhana hiyo ya kujitolea inakuwa haitekelezeki,” alisema.

Akifafanua kuhusu dhana ya kujitolea, Mapunda alisema kazi hiyo haifanywi kama ajira rasmi; inahitaji watu wa kujitolea wenye shughuli zao zingine za maendeleo.

“Kama kutakuwepo na utaratibu rasmi wa kupewa motisha kutoka nje ya mfuko wa mteja sina pingamizi na hilo, lakini kuchukua fedha au zawadi yoyote kutoka kwa mteja ili ahudumiwe, hilo ni jambo lisilokubalika kimaadili,” alisema

Reactions:

0 comments:

Post a Comment