Tuesday, 30 December 2014

WANAWAKE WATUHUMIWA KUWAZENGEA MAKASISI

Wanawake acheni kuzengea makasisi

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Mhashamu Yuda Thadeus Ruwa’ichi amewataka akina mama kuacha kuwazengea makasisi, hatua inayoweza kuwafanya kukacha kiapo chao cha useja.

Kwa mujibu wa Askofu Mkuu Ruwa’ichi, pamoja na baadhi ya akina mama ‘kuwazengeazengea’, kumekuwa na msukumo kutoka kwa baadhi ya waumini, kuwashawishi makasisi kuasi kiapo cha useja walichoapa ili wakaoe.

Akizungumza kabla ya kuwaweka wakfu mafrateli watano kuwa makasisi,
ambayo ni hatua ya mwisho kabla ya kuwa mapadri kamili, Ruwa’ichi alisema akina mama mnatakiwa kukaa mbali na watumishi hao wa Mungu.

“Jamani hawa vijana sasa wameingia katika hatua mpya ambapo sasa watakula kiapo cha kuishi maisha ya useja kwa muda wao wote wa utumishi wa kanisa, hivyo ni vema akina mama kukaa mbali nao sasa,” alisema wakati wa mahubiri katika viwanja wa Kawekamo eneo la Pasiansi jijini hapa.

Ingawa alionekana kutoa ujumbe kwa njia ya utani, lakini alisisitiza baadae kuwa limekuwepo ongezeko kubwa la waumini kujitokeza kwa viongozi wa kanisa, kuwaombea ndugu zao mapadre waoe na kwa hiyo kuachana na kiapo cha useja, jambo ambalo ni kinyume na msimamo wa Kanisa Katoliki pote duniani.

Askofu Ruwa’ichi alisema siku moja kabla ya misa ya kuwekwa wakfu, alikaa na mafrateri hao na kukumbushana mambo ya msingi na msimamo wa kanisa juu ya utumishi wao, likiwamo kuzingatia bila kutetereka kiapo cha useja.

Badala ya kuwaongoza kutenda kinyume na msimamo wa kanisa, Askofu Mkuu aliwataka waumini kuwaombea vijana hao ili waweze kuishi viapo vyao na kulitumikia kanisa kwa mujibu wa mafundisho ya Bwana Yesu, ambaye dunia hivi sasa inaadhimisha kuzaliwa kwake.

Kuhusu dhana kuwa mapadri wako kwenye hatari ya kufa bila kuzaa watoto kama wengi wa wanaojitokeza kuwaombea kuoa wamekuwa wakidai, Baba Askofu Mkuu alisema kwa mapadri kutumikia vizuri kanisa, wanazaa watoto wengi zaidi, ambao ni wafuasi wa kweli wa Yesu na mafundisho yake.

Aliwataka waumini kujiandaa kuadhimisha hitimisho la mwaka wa familia hapo tarehe 22 Machi mwakani na kwamba siku hiyo itakuwa siku maalumu ya kuziombea familia ili ziweze kuishi maisha matakatifu yanayompendeza Mungu.
Awali, wazazi wote wawili waliwasindikiza watoto wao mafrateri kwenda altare na kuwakabidhi kwa Baba Askofu wakila kiapo kwamba wameridhia kwa hiari yao kuwaachia wafanye kazi ya kumtumikia Mungu na kanisa lake.

Askofu Ruwa’ichi alisema kimsingi mashemasi, mapadri na maaskofu sio ‘mabwana wakubwa’ kama inavyoweza kutafsirika kwa baadhi ya waamini, bali wanahitaji sala na kila msaada wa wana wa mungu ili waweze kuyaishi maagano yao bila kutetereka.

Mafrateri waliowekwa wakfu na kuwa Makasisi ni na Frateri Stanslaus Rupia, Frateri John Makungu, Frateri Carol Rubinza, Frateri Onesmo Ngelwa na Frateri Canisius Milango ya Batemi.Baadhi ya waumini waliozungumza na gazeti hili baada ya misa walimpongeza Baba Askofu kwa kuzungumzia kwa uwazi juu ya shinikizo kwa kanisa, kuwaruhusu mapadre kuoa wakisema ndoa waliyofunga na kanisa tayari inatosha.
chanzo; habarileo.co.tz

Reactions:

0 comments:

Post a Comment