Sunday, 28 December 2014

GEOFREY MUNGAI AWAPA GOOD TIME WATOTO YATIMA WA DAILY BREAD LIFE CHILDREN'S HOME

Geofrey Mungai akionesha upendo kwa mtoto huyu yatima
Wakipata chakula pamoja na watoto wa kituo hicho
Angalia, watoto hawa walivyopendeza, ili waendelee vizuri wanahitaji msaada wako na wangu
Ni kama tunafanana, lakini kiuharisia huyu sio mwanangu, ndivyo anavyoonekana Sarah Mungai akisema kuhusu mtoto huyo yatima anayehitaji msaada wako
Mchungaji Mpeli akishukuru kwa msaada wa Mungai
Sarah Mungai akisoma risala ya mumewe
MFANYABISHARA maarufu wa mjini Iringa, Geofrey Mungai, amewawezesha  watoto yatima wa kituo cha Daily Bread Life Children’s Home kusheherekea vizuri siku kuu ya Krismas na kuukaribisha mwaka mpya, 2015 kwa kuchangia zaidi ya Sh Milioni 2.

Kiasi hicho cha fedha kimewawezesha watoto hao zaidi ya 39 wa kituo hicho kilichopo Mkimbizi, mjini Iringa kupata vyakula mchanganyiko na vinjwaji mbalimbali baridi wakati wa siku kuu ya Krismasi na nguo mpya walizofaa siku hiyo na watakazovaa Januari 1, 2015.

“Watoto hawa wanawakilisha kundi kubwa la watoto wenye sifa kama zao ambao kama jamii inayowazunguka haitakuwa jirani nao, kuwaonesha upendo na kuwapa misaada muhimu wanayohitaji, ndoto zao za maisha zinaweza kupotea,” alisema Mungai baada ya kutoa msaada huo hivikaribuni.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na mkewe, Sarah Mungai, Mungai alisema baada ya kusaidia watoto hao kwa miaka kadhaa iliyopita, hivisasa anaona jambo hilo kama wajibu wake anaotakiwa kuutekeleza kila mwaka.

“Nimejifunza mahitaji ya watoto hawa na moja ya hitaji lao muhimu ni upendo toka kwa watu wanaowazunguka kwa kuzingatia kwamba hawakupenda wazaliwe katika mazingira waliyonayo,” alisema na kutoa wito kwa wengine kushiriki kuzishughulikia changamoto zao.

Akimpongeza Mungai kwa mchango wake kwa watoto hao, mkurugenzi wa shirika la Daily Bread Life Tanzania linaloendesha kituo hicho, Mchungaji Mpeli Mwaisumbi alisema: “wakipata mahitaji yao muhimu na haki zao za msingi, watoto hawa, wenye malengo mengi katika maisha yao, wanaweza kuwa chachu ya maendeleo ya Taifa hili.

“Kwa bahati mbaya wakiwa katika mazingira kama haya wengi wetu tunadhani kati yao, hatuwezi kupata wasomi waliobobea na wanaoweza kushika nafasi nyeti za uongozi katika Taifa hili,” alisema.

Alisema ili watoto hao wafikie ndoto walizonazo katika maisha yao ni muhimu wakapata mahitaji yao mbalimbali kama ilivyo kwa watoto wengine na akarudia kutoa wito kwa wenye nafasi kuwakumbuka kwa kile alichosema wanapofanya hivyo wanaongezewa baraka za Mungu.


Tangu kuanzishwa kwake mkoani Iringa 2004 mbali na kuendesha kituo hicho cha watoto yatima, Shirika la Daily Bread Life Tanzania linaendesha pia kituo cha watoto yatima cha Nzihi chenye watoto 24 huku likitoa msaada kwa watoto 241 walio nje ya shule katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya na Iringa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment