Tuesday, 4 November 2014

VIGOGO TPDC WATIWA MBARONI

Vigogo TPDC watiwa mbaroni

Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Michael Mwanda na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, James Andilile jana walikamatwa na polisi kwa agizo la na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), inayoongozwa na Zitto Kabwe kwa kushindwa kuwasilisha mikataba 26 ya gesi na mapitio yake mbele kamati hiyo tangu mwaka 2012.

Baada ya kukamatwa, Mwanda na Andilile walipandishwa katika gari dogo la wazi (pick-up) la polisi na kupelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi ambako taarifa iliyotolewa baadaye jioni na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova ilisema viongozi hao wameachiwa huru kusubiri sheria na taratibu za Bunge.

Kamanda Kova alisema baada ya kuwakamata ilibainika kwamba katika Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 Kifungu cha 12 (3) kinamtaka Mwenyekiti wa PAC kupendekeza kwa Spika wa Bunge kwanza kuhusu jambo lolote aliloliona kama ni kosa.

“Spika akisharidhika kuhusu tuhuma zozote zilizoletwa mezani kwake ndipo anamwandikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili suala hilo lipate ufafanuzi wa kisheria ikiwa ni pamoja na hatua za kisheria zinazostahili kuchukuliwa.

Tofauti na vikao vya kamati za Bunge, kikao hicho cha PAC kilichofanyika katika Ofisi Ndogo ya Bunge, Dar es Salaam jana kiliwaapisha wakuu hao wa TPDC kazi iliyofanywa na Mwanasheria wa Bunge, Nenelwa Mwihambi na chumba cha mkutano huo kikiwa kimezungukwa na polisi watano waliovalia sare ambao ndiyo waliowatoa vigogo hao na kuwapakia katika gari.

Jumatatu iliyopita, vigogo hao walitimuliwa katika kamati hiyo baada ya kushindwa kuwasilisha mikataba hiyo na kutakiwa kufanya hivyo baada ya siku mbili na baadaye kuongezewa hadi tano, bila mafanikio.

Katika utetezi walioutoa wiki iliyopita, viongozi hao walisema kwa mujibu wa taratibu, mikataba hiyo inatakiwa kupitia Ofisi za Bunge na si katika kamati.

Jana, waliieleza kamati hiyo kwamba wameshindwa kuiwasilisha kwani kwa nyakati tofauti, wamewasiliana na Wizara ya Nishati na Madini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Frederick Werema na kujibiwa kuwa mikataba hiyo haitakiwi kuonyeshwa hadharani.

Walisema kwa mujibu wa maelezo ya AG, mikataba hiyo ikiwekwa wazi, inaweza kuifanya Serikali ifunguliwe kesi na wawekezaji.

Kabla ya kuanza kwa kikao hicho, Mwihambi alianza kwa kusoma Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge, Sura ya 296 inayoeleza mamlaka ya Bunge au kamati kuagiza nyaraka yoyote inayotaka kutoka kwa mtu yeyote kwa ajili ya utekelezaji wa kazi yake, isipokuwa nyaraka inayohusiana na masuala ya kijeshi, ambayo hutolewa kwa kibali cha Rais.

“TPDC iliagizwa kuleta nyaraka za mikataba 26 tangu Januari 26, 2012. Kwa kipindi chote hicho katika mawasiliano kati ya TPDC, Kamati na Katibu wa Bunge, hakuna maelezo yoyote ambayo yamewahi kutolewa kuwa mikataba hiyo inahusiana na masuala ya kijeshi,” alisema.

Akitoa ufafanuzi Zitto alisema: “Kamati imetumia mamlaka yake ya kulazimisha maagizo yake kutekelezwa na pale ambapo maofisa wa Serikali wanashindwa kutekeleza, PAC ina mamlaka ya kuchukua hatua za kisheria kama tuliyochukua.”

Aliongeza: “Tumewapeleka polisi maofisa wa umma wanaoshindwa kutekeleza maagizo ya Bunge kwa mujibu wa Sheria ya Kinga na Madaraka ya Bunge Kifungu cha 12 cha Sheria Namba 3 ya mwaka 1988.”

Alisema PAC iliomba mikataba hiyo kwa sababu kwa muda mrefu, kumekuwa na kilio cha Watanzania juu ya usiri wa mikataba... “Bunge au kamati zake zina mamlaka ya kufahamu mikataba ya Serikali kwa masilahi ya wananchi.”

Wakijitetea, vigogo hao walisema kisekta wanawajibika kwa Wizara ya Nishati na Madini na kisheria, wanawajibikwa kwa AG.

Ifuatayo ni sehemu mazungumzo kati ya Zitto na Kaimu Mkurugenzi wa TPDC:
Zitto: Kwa nini TPDC katika majibu yake imeeleza kwamba inafuata maagizo ya AG badala ya kamati?

Kaimu Mkurugenzi: Sina utaalamu wa kisheria na AG ndiyo anaweza kuzifafanua sheria na hilo ni suluhisho alilolitoa.

Zitto: Masilahi ya kibiashara ya wananchi yanalindwa na nani. Una jibu katika hili?

Kaimu Mkurugenzi: Sina jibu. Sina jibu kwa sababu AG ametafsiri katika barua yake na siwezi kumsemea.

Zitto: Katika barua uliyomuandikia Katibu wa Bunge tena ukipigia mstari majibu yake, ulisema mwongozo wa AG unapaswa kuzingatiwa, hayo ndiyo maoni ya TPDC na mnalielekeza Bunge kuzingatia maoni ya AG?

Kaimu Mkurugenzi: Masilahi ya nchi yanalindwa na wanaosimamia sheria husika ambao ndiyo wanaingia katika mikataba husika.

Zitto: Katika maoni uliyosema tuyazingatie, umesema mikataba ni ya siri na wawekezaji wasingependa iwekwe wazi katika Kamati za Bunge. Unakubaliana na mwongozo wa AG mpaka ukamuomba Katibu wa Bunge auzingatie.

Kaimu Mkurugenzi: Ndiyo.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment