Wednesday, 5 November 2014

RAIS APIGA MARUFUKU KAMPENI YA KATIBA INAYOPENDEKEZWA


Wakati Rais Jakaya Kikwete akipiga marufuku vyama vya siasa na asasi za kiraia kufanya mapema kampeni za kuhamasisha wananchi kuhusu Katiba Inayopendekezwa, Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umenasa waraka wa mkakati wa kutumia Sh2.5 bilioni za umma kuipigia debe katiba hiyo.

Pamoja na kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa jana wakati akilihutubia Taifa kupitia wazee wa Dodoma, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein jana hiyohiyo, aliwataka Wazanzibari kuipitisha Katiba Inayopendekezwa bila kufanya makosa.

Nyuma ya kauli hizo za marais, Ukawa umesema umeandaliwa mkakati kabambe wa kuvitumia vyombo vya habari kwa fedha za umma kutoka Ikulu kuwashawishi wananchi kupigia kura ya ‘ndiyo’ katiba hiyo.

Kauli ya Rais Kikwete
“Kwa sababu hiyo naomba Watanzania wenzangu tuzingatie mamlaka ya Sheria ya Kura ya Maoni ambayo imeelekeza vizuri lini kura ya maoni itafanyika na lini kampeni zitafanyika, lini wadau watatoa elimu naomba tuwe na subira. Tukizingatia sheria hii hakuna ugomvi.”

Aliongeza hadi Tume itakapotoa maelekezo ya utekelezaji, wakati wa kampeni na kutoa elimu kwa umma bado na kwamba sheria ipo na imezipanga siku maalumu za kufanya hivyo.

Alisema licha ya sheria kuruhusu kampeni kufanyika ndani ya siku 60 kabla ya kura za maoni kupigwa, kwa mamlaka yake akiwa kiongozi wa nchi, kura na kampeni vitafanyika ndani ya siku 30 tu.

“Kampeni zitaanza tarehe 30 Machi na kumalizika tarehe 29 Aprili ikiwa ni siku moja kabla ya kupiga kura ya maoni. Muda huo ndiyo utakuwa wa kufanya hivyo,” alisema Kikwete.

Dk Shein aipigia debe
Wakati Kikwete akisema hayo, Dk Shein amesema Katiba Inayopendekezwa ni mwarobaini wa kero nyingi za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na Wazanzibari wasifanye makosa kuikataa wakati wa kura ya maoni mwakani.

Akizungumza katika kongamano la kuadhimisha miaka minne ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Dk Shein alisema iwapo Katiba hiyo itapitishwa, itasaidia kuimarisha Muungano kwa kuwa imezingatia makubaliano ya Muungano ya kuwa na Serikali mbili.
chanzo; mwananchi


Reactions:

0 comments:

Post a Comment