Sunday, 9 November 2014

NAIBU WAZIRI, FINLAND WAZINDUA RASMI PROGRAMU YA PANDA MITI KIBIASHARA

Naibu Waziri wa Maliasilia na Utalii Mahamudu Mgimwa na Mwakilishi wa Balozi wa Finland, Mikko Lappanen wakinyosha mikono kuashiria uzinduzi wa programu mpya ya panda miti kibiashara
Mgimwa akipanda mti mmoja wa mfano katika viunga vya ofisi mpya za halmashauri ya mji wa Njombe
Mwakilishi wa Balozi wa Finland, Mikko Lappanen naye alipanda wa kwake
Aliyekuwa katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii (sasa Sheria na Katiba), Maimuna Tarishi pamoja na mwakilishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Gladness Mkamba nao walipanda miti yao 
Mkurugenzi wa Panda Miti Kibiashara, Dk Maria Tham naye alipanda wa kwake
Kisha wakubwa hao wakalifuata jiwe na msingi na kuzindua rasmi programu hiyo
Wakati shughuli hiyo ikiendelea kulikuwa na burudani pia
Hawa waliimba na kuigiza umuhimu wa kupanda miti kibiashara
Mwakilishi wa balozi wa Finland, Leppanen akasema neno
Bango linalooelezea programu hiyo
Mzee George Matiku ambaye ni mmoja wa maafisa wa programu hiyo ndiye aliyeongoza sherehe ya uzinduzi
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, mahamudu Mgimwa ameizindua rasmi Programu ya Panda Miti Kibiashara (PFP) inayolenga kuongeza kipato kwa wananchi huku akiwataka wakulima kujiunga katika vikundi ili kunufaika nayo.

Mkurugenzi wa PFP, Dk Maria Tham alisema katika halfa hiyo kwamba programu hiyo inatekelezwa katika wilaya sita za mikoa ya Iringa, Njombe na Morogoro.

Dk Tham alizitaja wilaya hizo kuwa ni pamoja na Makete, Njombe na Ludewa kwa mkoa wa Njombe, Kilolo na Mufindi kwa mkoa wa Iringa na Kilombero kwa mkoa wa Morogoro.

Alisema kwa kupitia program hiyo wakulima watawezeshwa ili wapande miti kitaalamu kwa kutumia mbegu bora na kuhudumia mashamba yao ipasavyo kwa kuzingatia mipango endelevu ya ardhi.

Akizindua program hiyo kwa kuweka jiwe la msingi, alisema program hiyo inatekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya mambo ya Nje ya Finland.

Mgimwa alisema tangu miaka ya thamanini, serikali ya Finland imeendelea kutoa mchango mkubwa katika kuendeleza sekta ya misitu nchini.

Kwa kujua umuhimu wa misitu, Mgimwa alisema Finland ilifadhili pia uundwaji upya wa sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998 na sheria ya misitu na program ya Taifa ya Misitu na Nyuki.

“Ndugu wananchi, sasa mnachotakiwa kufanya chini ya program hii ni kupanda miti kibiashara. Nimeelezwa kuwa katika program hii mnao wataalamu waliobobea katika taaluma ya kupanda miti kibiashara kutoka Finland na hapa nchini,” alisema.

Mwakilishi wa ubalozi wa Finland nchini, Mikko Leppanen alisema serikali ya Finland ilikubaliana na serikali ya tanzani kuanzisha program hii katika maeneo hayo kwa kuwa wananchi wake wanajituma sana kupanda miti.

“Nachukua fursa hii na mimi kusema kuwapongezeni wananchi kwa kupanda miti kwa wingi na kusema ukweli mnaongoza hapa Tanzania kwa kupanda miti, hongereni sana. Nawatakieni mafanikio katika kilimo cha miti,” alisema.

Leppanen aliwataka wananchi wa mikoa hiyo kuipokea program hiyo kwa mikono miwili na kutekeleza yale watakayofundishwa na wataalamu ili waweze kupata manufaa makubwa kuliko yale wanayoyapata sasa.

Mkurugenzi wa PFP  alisema wananchi wanaopanda miti watahamasishwa kujiunga katika vikundi vya wakulima wa miti kwa nia ya kufanikisha utekelezaji wa program hiyo.

Dk Tham alisema katika kipindi cha miaka minne kuanzia sasa wananchi wa wilaya hizo watahamasishwa kupanda miti katika eneo lenye ukubwa wa hekta 15,000.

“Huku wakihimizwa kuanzisha shughuli mbalimbali za kujiongezea kipato wakati wakisubiri miti yao ikue na kufikia umri unaofaa kuvunwa,” alisema.

Alisema wakulima wanatakiwa kuingiza katika shughuli hiyo kwa kasi huku wakifahamu kwamba biashara ya miti itaongezeka ifikapo 2025 kwa kuzingatia kwamba mahitaji ya malighafi hiyo viwandani na kwa matumizi mengine majumbani yataongezeka kutoka mita za ujazo milioni 1.5 hadi milioni 3.7.

Wengine waliohudhuria uzinduzi wa program hiyo ni pamoja na wakuu wa mikoa na wilaya za mradi, wananchi na wawakilishi wa vikundi vya wakulima, wizara, PFP na ubalozi wa Finland,

Reactions:

0 comments:

Post a Comment