Tuesday, 11 November 2014

MKUU WA MAJESHI AMPA BIG UP KIKWETE, AWASIHI VIJANA WASIKUBALI KUPOTOSHWA KIFIKRA

 
Mkuu wa Majeshi, Jenerali david Mwamunyange alipokuwa JKT Mafinga, kikosi namba 841 KJ
Akizindua meza ya mchanga
Akiangali picha ya mabweni mapya
Akizindua mabweni
Mkuu wa Kikosi cha JKT Mafinga, Martin Mkisi naye alizungumzia changamoto za kikosi chake
Mkuu wa JKT Taifa, Raphael Muhunga naye akazungumzia mafanikio ya JKT
Baadaye akazindua jengo la burudani
Sehemu ya jengo hilo linavyoonekana
akisalimiana na mzabuni katika kikosi hicho mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka
Akiangalia kwa nje moja ya mabweni mapya
Kulikuwepo na burudani toka kwa vijana wa kujitolea
Wakiwa katika hali ya ukakamavu
MKUU wa Majeshi, Jenerali David Mwamunyange amemsifu Rais Jakaya Kikwete akisema ni “shupavu” huku akiwataka vijana waogope kupotoshwa kimawazo na kifikra ili wawe wazalendo.

Jenerali Mwamunyange aliyasema hayo juzi katika ziara yake ya siku moja aliyoifanya katika kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) namba 841 KJ, Mafinga, mkoani Iringa.

Akiwa katika kambi za kikosi hicho Mkuu wa Majeshi alizindua jengo la meza ya mchanga, mahanga mapya matano ya vijana na jengo la burudani lililojengwa Kinyanambo mjini Mafinga ambako nje kidogo ya kambi ya kikosi hicho.

“Kikwete ni Rais shupavu kabisa na sehemu ya ushupavu wake ameuonesha kwa kuviimarisha vikosi vya ulinzi na usalama likiwemo jeshi la kujenga Taifa,” alisema.

Alisema mchango wa JKT katika kuboresha malezi ya vijana ni wa dhahiri na unaotakiwa kudumishwa ili kuwaandaa vijana wa taifa hili na la kesho.

“Ukitaka kuona Taifa la kesho litakuwaje, angali vijana wanavyolelewa hii leo. Kwahiyo ule usemi wa mtoto umleavyo ndivyo akuavyo ni lazima uzingatiwe kwa maslai ya taifa,” alisema.

Jenerali Mwamunyange alisema; “ukiwaacha vijana wapoteshwe kimawazo, kifikra na kwa namna yoyote ile basi ujue unatengeneza taifa lisilo imara, la vijana wasio wazalendo, wenye upendo, mshikamano na ambao hawatakuwa tayari kutetea na kulinda amani ya nchi yao,” alisema.

Alisema mafunzo ya JKT ni muhimu kwa vijana na watu wa kada mbalimbali bila kujali dini, rangi, kabila na wanakotoka kwani yanasaidia sana kuwaanda raia kuwa wazalendo, wanaopendana, wenye mshikamano na wenye uchungu na taifa lao.

“Mbali na kuwaandaa rai kuwa wazalendo, ni jeshi linalowafundisha watanzania kujitegemea kwa kufuga, kulima na kufanya shughuli mbalimbali za ujasiriamali,” alisema.

Jenerali Mwamunyange aliwasihi watanzania waliopitia JKT na vijana wanaoendelea kujiunga na jeshi hilo kuyatumia mafunzo waliyopata kuiendeleza misingi iliyoachwa na waasisi wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Amani Abeid Karume.

“Misingi hiyo ni amani, upendo na mshikamano. Wajibu wetu ni kuiendeleza na tukifanya hivyo tutaonesha uzalendo kwa nchi yetu,” alisema.

Akizindua meza ya mchanga, mkuu wa majeshi alisema meza hiyo inasaidia kutambua na kulinda mipaka ya kikosi kutokana na kuwepo kwa changamoto ya kuvamiwa na raia kutokana na ongezeko la watu pamoja na kupanuka kwa shughuli za kijamii.


Katika ziara hiyo, Mwamunyange alilakiwa na Mkuu wa JKT Taifa, Meja Jenarali Raphael Muhunga, kamanda wa kikos cha JKT Mafinga Luteni Kanali Martin Mkisi, makamanda wa vikosi, maafisa wakuu, maafisa wadogo, askari, vijana na watumishi wa umma.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment