Sunday, 2 November 2014

MKURUGENZI AWATIMUA WANAHABARI KATIKA KIKAO CHA BARAZA LA MADIWANI


MADIWANI wa Halmashauri wa Wilaya ya Muleba mkoani Kagera wamelaani kitendo cha Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Joseph Mkude kuwafukuza waandishi wa habari na wananchi katika vikao vya Baraza la Madiwani hao.

Madiwani hao wamedai kuwa Mkurugenzi huyo amekiuka kanuni ya kudumu namba 12 kifungu (1) na cha (2) inayowaruhusu kuhudhuria vikao hivyo vya wazi.

Madiwani hao ambao walitishia kususa na kuahirishwa kwa kikao cha baraza cha juzi, walimtaka mkurugenzi huyo kurejea matangazo yake aliyoyaweka katika mbao za matangazo za halmashauri hiyo yaliyowatangazia wananchi kufanyika kwa mkutano wa baraza la madiwani na kuwakaribisha kusikiliza kinachojadiliwa.

Hali hiyo ya madiwani kumtaka Mkude arejee matangazo yake ilikuja baada ya Mkurugenzi huyo kuingia katika ukumbi wa vikao na kuwataka baadhi ya wananchi pamoja na waandishi wa habari waliokuwa wamehudhuria kuondoka.

Alisema, “nimepata tetesi kuwa wamo waandishi wa habari katika kikao hiki cha baraza dogo la kujadili taarifa za kata hususani zinazohusu ujenzi wa maabara ambazo huwasilishwa na kila diwani wa kata au mtendaji.

“Sasa, nawataka watu wote wasiokuwa watendaji wa halmashauri hasa waandishi wa habari kuondoka mara moja kabla sijachukua hatua kwani ni lazima mkaandike habari za Muleba? Ondokeni hiki ni kikao changu cha kazi.”

Kauli hiyo iliwafanya waandishi wa habari waondoke na kwenda katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Lembris Kipuyo na kumweleza yaliyojiri ambapo Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka kuwa wavumilivu wakati yeye akiendelea kulishughulikia suala hilo.

Siku moja baadaye baada ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, George Katomelo kufungua kikao na kutaka wapitishe ajenda za kikao hicho, madiwani waliinua mikono wakimtaka Mwenyekiti awape nafasi kabla ya kupitisha ajenda hizo ili watoe dukuduku lao.

Mwenyekiti huyo alimuinua Diwani wa Kata ya Kishanda aseme kwa niaba ya wenzake ambapo diwani huyo Alfred Pastory alisema hawawezi kuendelea na vikao kama Mkurugenzi hatatoa majibu kwa mambo ambayo walimtaka atoe majibu yake au kikao kiahirishwe.
“Tulikuagiza (Mkurugenzi) utufafanulie kwa nini unafukuza waandishi wa habari katika kikao cha wazi umetumia kanuni ipi, ajenda nyingine unatuletea leo asubuhi siku ya kikao wakati kikanuni zinaeleza zinapaswa kuletwa siku saba kabla ili tuzisome na kuzielewa sasa kama hayo hayana majibu basi kikao kiahirishwe,” alisema.

Diwani mwingine wa Kata ya Bumbile, Sweetbart Mutembei alisema kukimbia tatizo si utatuzi wake, kwa hiyo wakae pamoja na kuyamaliza huku akisema kuwafukuza waandishi na wananchi ni kukiuka kanuni ya kudumu ya 12 kifungu cha kwanza na cha pili kinachosema kuwa mikutano ya baraza itakuwa wazi kwa wananchi na waandishi wa habari ambapo halmashauri itatangazia umma kuhusu muda.

Kwa upande wake Mkurugenzi huyo, aliwaomba waandishi wa habari kukutana naye ofisini kwake ili waweze kuzungumza ambapo waliitikia mwito. Baada ya kuingia ofisini kwake, Mkurugenzi huyo alisema;

“Nina mwongozo wangu niliojiwekea kuwataka mje kwenye vikao au kuwafukuza, eleweni mimi ndiye mwenye nyumba mpya waliokuwepo wa zamani wana utaratibu wao eti wanafuata kanuni za kudumu, mimi nina zangu, nimewaita kuwaeleza kuwa nilichofanya jana kuwafukuza nyie na wananchi nina uhakika nacho, sitaki ushirikiano.“Waulizeni hata waandishi wa habari nilipotoka Iringa, walikuwa wakilitambua hilo msije mkathubutu kuingia kwenye vikao vyangu vya baraza mpaka niwaite mimi, mtu yeyote ambaye yuko chini yangu akiwaita waandishi nitamwajibisha,” alisema na kuwaacha waandishi ofisini kwake na yeye kurudi kwenye kikao.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment