Tuesday, 4 November 2014

MDADA WA IRINGA, CHRISTINA KIGAHE APANDISHWA KIZIMBANI AKIHUSISHWA NA BIASHARA YA DAWA ZA KULEVYA

Picha ya mtandaoni ya Christina Kigahe

Mfanyabiashara na mkazi wa Mikocheni, Christina Kigahe (36) jana alipandishwa katika kizimba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka matatu ya kuingiza nchini dawa za kulevya zenye thamani ya zaidi ya Sh99 milioni.

Wakili wa Serikali, Janeth Kitali alidai mahakamani hapo kuwa Desemba 11, 2013, mshtakiwa alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akiingiza nchini gramu 1227.37 za dawa za kulevya aina ya Heroine Hydrochloride zenye thamani ya Sh55,231,650.

Kitali alidai kuwa siku hiyo ya tukio, mshtakiwa huyo pia alikamatwa akiingiza nchini gramu 670.06 za dawa za kulevya aina ya Heroine Hydrochloride zenye thamani ya Sh30,152,700.

Alidai kuwa Chritina siku hiyo hiyo ya tukio pia alikamatwa akiingiza kiasi kingine cha dawa za kulevya aina ya Heroine Hydrochloride kiasi cha gramu 310.02 chenye thamani ya Sh13,950,900.

Hata hivyo, mshtakiwa aliyakana mashtaka hayo na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na hivyo kuomba kesi hiyo ipangiwe tarehe nyingine ya kusikilizwa.

Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda alimtaka mshtakiwa huyo kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao kila mmoja atasaini bondi ya Sh2 milioni na aliiahirisha hadi Novemba 17, mwaka huu. Aliachiwa kwa dhamana.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment