Tuesday, 4 November 2014

KILA KATA IRINGA MJINI KUWA NA MSAIDIZI WA KISHERIA

Sidified Mapunda
washiriki wa mafunzo
Mmoja wa wawezeshaji Aidan Mkusa
KATA 16 za Manispaa ya Iringa zinatarajia kupata wasaidizi wa kisheria (Paralegals) baada ya kituo cha Msaada wa Kisheria Iringa (Iringa Paralegal Centre) kuanza kutoa mafunzo kuhusiana na mpango huo.

Kila kata imetoa mtu mmoja atakayeshiriki mafunzo hayo yaliyoanza jana na yatakayofanyika kwa siku tano katika ukumbi mdogo wa IDYDC mjini hapa kwa ufadhili wa asasi ya Legal Services Facility ya Denmark.

Mratibu wa Kituo cha Msaada wa Kisheria Iringa, Sidified Mapunda alisema wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo kwamba watakapohitimu, washiriki hao watambue kwamba wataifanya kazi hiyo kwa kujitolea.

“Hii ni kazi ya kujitolea inayoweza kufanywa na mtu yoyote yule mwenye kiwango cha elimu kuanzia kidato cha nne na kuendelea,” alisema.

Aliyataja majukumu ya wasaidizi wa kisheria kuwa ni pamoja na kutoa msaada wa kisheria, kuelimisha jamii haki zao kisheria na kuelekeza jamii juu ya vyombo mbalimbali vya kupata haki kama Polisi, mahakama na mabaraza ya usuluhishi ya kata.

Zingine ni pamoja na kusaidia kutatua migogoro katika jamii ambayo sio lazima ipelekwe kwenye vyombo vya dola na kuwaandalia wateja hati au nyaraka za kisheria pale inapowezekana.

Mapunda alisema wasaidizi wa kisheria hawatakiwa kudai gharama zozote kutoka kwa wateja wao kwa kuwa wamekubali kuifanya kwa kujitolea.

“Baada ya mafunzo haya msije walaghai wateja wenu kwa kujiita nyie ni wanasheria au mawakili na kuanza kutoza gharama za ushauri kama wanavyofanya mawakili,” alisema.

Alisema mpango huo unalenga kuwa na watu katika ngazi ya kata watakaowasaidia watu wengine kupata na kulinda haki zao bila kutumia gharama kubwa.

“Kwahiyo baada ya mafunzo haya, kutakuwa na awamu nyingine nne za mafunzo kama haya yatakayofanyika kwa awamu tofauti tofauti katika kipindi cha miaka miwili na nusu ijayo; lengo ni kuwawezesha kuifahamu dhana hii kwa ufasaha na kuwasaidia wenye uhitaji katika maeneo yenu ” alisema.

Washiriki wa mafunzo hayo wamesema mafanikio ya kazi hiyo yanaweza kuwa mara dufu kama wadau wataangalia uwezekano wa kuwalipa posho ya kila mwezi.

Katika mapendekezo ya kiasi gani wasaidizi wa kisheria walipwe kama motisha, mmoja wao aliyejitambulisha kwa jina la Jackson Haule alisema; “kwa mazingira ya sasa posho ya Sh 100,000 inaweza kutusaidia kuongeza ufanisi wa kazi hiyo.”

Alisema ili dhana ya kujitolea ina mipaka yake kwani watakapohitimu mafunzo hayo na kuanza kuitekeleza kazi hiyo wanafahamu kwamba watalazimika kuingia gharama mbalimbali ili kuifanikisha.

“Gharama hizo zinahusisha kusafiri kutoka eneo moja hadi jingine, kuchapisha nyaraka mbalimbali, gharama za mawasiliano na zinginezo na kama tukishindwa na wateja wetu wakatugharamia dhana hiyo ya kujitolea inakuwa haitekelezeki,” alisema.

Akifafanua kuhusu dhana ya kujitolea, Mapunda alisema kazi hiyo haifanywi kama ajira rasmi; inahitaji watu wa kujitolea wenye shughuli zao zingine za maendeleo.

“Kama kutakuwepo na utaratibu rasmi wa kupewa motisha kutoka nje ya mfuko wa mteja sina pingamizi na hilo, lakini kuchukua fedha au zawadi yoyote kutoka kwa mteja ili ahudumiwe, hilo ni jambo lisilokubalika kimaadili,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment