Tuesday, 28 October 2014

WANAUME WADAIWA KUCHANGIA BAADHI YA VIFO VYA WAJAWAZITO

Wanaume wadaiwa kuchangia vifo vya wajawazito

TABIA ya baadhi ya wanaume kuwatekeleza au kutowajali wajawazito wanaowahusu imeelezwa kusababisha baadhi ya vifo vyao.

Ingawa vifo vingi vinatokea hospitalini, ushuhuda wa baadhi ya wananchi na watumishi wa afya, unaonesha wapo wajawazito ambao matatizo huchangiwa na na ukosefu wa huduma bora nyumbani.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, mkazi wa kijiji cha Lowa kilichoko halmashauri ya manispaa ya Sumbawanga, Antonia Kawozya (70) alishuhudia kifo cha mjukuu wake aliyepoteza maisha hospitali ya mkoa hivi karibuni.

Aliwaambia waandishi pamoja na timu ya Muungano wa Utepe Mweupe wa Uzazi Salama Tanzania (WRATZ) kwamba, mjukuu huyo alikuwa akiishi kijiji cha Muza ambako inadaiwa akiwa na ujauzito, alitelekezwa na mumewe.

“Alikuja hapa nyumbani (Lowa) akiwa katika hali mbaya, tulimpeleka zahanati tukaambiwa kwa jinsi hali yake ilivyokuwa tumwahishe hospitali ya mkoa,” alisema Kawozya.

Kwa mujibu wa Ofisa Muuguzi na Mkunga katika hospitali ya mkoa wa Rukwa, Fides Nduasinde, alisisitiza wanaume hususani vijijini, kuwa chachu ya mabadiliko katika kukabili vifo vya wajawazito.

“Karibu kila sehemu nilipozungumza na wananchi, ilionekana kuna mfumo ambao haupendezi karibu kila familia. Mfumodume, akinamama wengi walilalamika kwamba hakuna uamuzi wowote kwenye familia unaweza kutolewa bila baba kuamua,” alisema.

Alisema likija suala la uchumi katika familia, unabebwa na baba kiasi kwamba inapotokea dharura, asipokuwa tayari kuamua, mjamzito anaweza kucheleweshwa au kutokwenda hospitalini.

Licha ya Ndusambile , pia katika mikutano kati ya wananchi na WRATZ kwenye halmashauri zote, baadhi ya wananchi walikiri kwamba mwenye uamuzi wa mjamzito kwenda kujifungua ni mwanamume kwa kuwa ndiye aliyeshikilia uchumi wa familia.Aidha, Nduasinde alikemea tabia ya waume kuachia watu wengine zaidi wazee, kusindikiza wajawazito kujifungua. Alisema kama ambavyo wamehamasishwa kusindikiza wake zao kliniki, ni vyema pia wakati wa kujifungua wafanye hivyo.
chanzo;habarileo

Reactions:

0 comments:

Post a Comment