Friday, 17 October 2014

WALIMU KILOLO WAICHOKONOA SERIKALI 
walimu Kilolo walivyoadhimisha siku ya mwalimu
DHARAU zinazooneshwa na baadhi ya watu dhidi ya walimu nchini zimeelezwa na Chama cha Walimu (CWT) wilaya ya Kilolo kwamba chanzo chake ni maslai duni wanayopata kutoka katika chanzo chake kikuu, serikali.

Chama hicho kimesema baadhi ya walimu wanashindwa kuripoti katika vituo vya kazi wanavyopangiwa na serikali na wakati mwingine kuamua kutafuta ajira nyingine kwasababu ya kukosa au kucheleweshewa stahiki zao.

Akizungumza hivikaribuni wakati wilaya hiyo ikifanya maadhimisho ya siku ya walimu, Mwenyekiti wa Chama wa Walimu (CWT) wilaya ya Kilolo, Yolanda Mgata alisema; “walimu wanafanya kazi katika mazingira magumu, wamekata tama, hawasikilizwi na kusababisha wafanye kazi kwa kinyongo hali inayodhorotesha maendeleo ya taaluma nchini.”

Kuhusu madai mbalimbali ya walimu dhidi ya mwajiri wao, Mgata alisema serikali imeendelea kuahidi kuyafanyia kazi kwa kasi inayozidi kuwakatisha tamaa walimu wanaodai.

Pamoja na walimu kuendelea kupuuzwa na mwajiri wao alisema CWT itaendelea na majadiliano na serikali kuhusu nyongeza ya mishahara na marupurupu mengine.

“Tunatoa wito kwa serikali kukutana haraka na CWT ili kuendeleza majadiliano ya hoja mbalimbali zinazolenga kuboresha maslai ya mwalimu nchini,” alisema.

Alisema walimu wamechoshwa na kauli za mara kwa mara zinazotolewa na serikali kwamba ina nia ya kuboresha maslahi yao kwani tangu ianze kutoa ahadi hiyo kasi ya utekelezaji hairidhishi.

Pamoja na madai waliyonayo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilolo, Yusuph Msawanga aliwataka walimu kuzingatia kanuni na taratibu za kazi katika utendaji wa kazi.

“Ni vema mkatimiza wajibu wenu kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili msiingie kwenye migogoro ya kikazi isiyo ya lazima; hiyo itawasaidia msichukuliwe hatua za kisheria wakati mkidai haki zenu,” alisema. 

Katika risala yao walimu hao walisema kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni marekebisho ya mishahara baada ya kupandishwa vyeo na kuchelewa malipo ya malimbikizo baada ya kurekebishwa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment