Saturday, 4 October 2014

WADAU IRINGA WAANDAMANA KUPINGA MAUAJI YA TEMBO NA FARU


baadhi ya wadau wakiwa wameshikilia bango baada ya maandamano hayo
Kaimu Mhifadhi Ruaha, Paul Banga
Mratibu wa SPANEST, Godwell Ole Meing'ataki
Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa (MP Chadema)
Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Iringa, Adam Swai
Burudani pia zilikuwepo
Katika picha ya pamoja
WADAU wa uhifadhi na utalii wa mkoa wa Iringa, leo hii wamefanya maandamano ya Tembo na Faru wakiungana na mataifa mengine duniani kuihamsisha jamii kushiriki mapambano ya kuwanusuru wanyama hao wanaozidi kupungua dhidi ya ujangili.

Maandamano hayo yaliyofanywa kwa uaratibu wa Taasisi ya Wildlife Connection, yalianzia benki ya Barclays mjini hapa, yakapita zilipo ofisi za Manispaa ya Iringa na kuelekea hadi uwanja wa Mwembetogwa.

Waziri Kivuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) aliitaka serikali kubeba jukumu la kuadhiimisha siku hiyo ili kuyapa maandamano hayo umuhimu mkubwa.

“Sio jambo la kujivunia kuendelea kuangalia maandamano haya yakifanywa na taasisi za kigeni wakati wanyama hao ni mali yetu na wana umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya nchi,” alisema.

Alisema serikali inatakiwa kuitangaza vya kutosha shughuli hiyo kama sehemu ya mikakati yake ya kupambana na ujangili wa wanyamapori nchini.

Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Iringa, Adam Swai aliyapongeza maandamano akisema yanaunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali na wadau wake katika kuhifadhi wanyama hao.

“Kuna umuhimu mkubwa sana kwa umma na wananchi kwa ujumla kutambua nafasi yao na kushiriki kikamilifu katika jitihada za kulinda wanyamapori na maliasili zetu tulizonazo kwa faida ya taifa kwa sasa na hata vizazi vijavyo,” alisema.

Naye Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST), Godwell Ole Meing’ataki alisema wanyama wana mchango mkubwa katika ukuaji wa sekta ya utalii na uchumi wan chi.

“Kwa bahati mbaya, tukiwa katika hali ambayo utalii bado haujukua vya kutosha katika mikoa ya Kusini, wanyama hawa wanazidi kuuawa kwasababu meno yake ni biashara kubwa nje ya nchi,” alisema.

Alisema meno ya tembo na faru yanasafirishwa kwenda katika nchi zenye mahitaji makubwa na bidhaa hizo kupitia barabara, mipaka, bandari na viwanja vyetu vya ndege.

Alisema meneo hayo yanatarajiwa kuwa na ulinzi unaoweza kubaini biashara hiyo halamu lakini tofauti na matarajio ya wengi men ohayo yanapita bila vikwazo.

Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Paulo Banga alisema Idadi ya Tembo katika hifadhi ya Ruaha imeshuka kutoka tembo 31,000 mwaka 2009 hadi 20,000 mwaka huu.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment