Tuesday, 21 October 2014

SIMUHOFII YOYOTE KINYANG'ANYIRO CHA URAIS 2015- JANUARI MAKAMBA

Januari Makamba akifafanua
Mbele ya wanahabari
NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba amesema hakuna mwanasiasa yoyote anayemuhofia kuwa kikwazo katika harakati zake za kuwania urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kutangaza nia hiyo April mwaka huu.

Makamba alitangaza nia hiyo alipokuwa akihojiwa katika kituo cha Dira ya Dunia kinachorushwa na kituo cha Televisheni cha Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Katika mahojiano maalumu aliyofanya jana na wawakilishi wa vyombo mbalimbali vya habari wa mjini Iringa waliotaka ufafanuzi kuhusu nia yake hiyo Makamba alisema; “huu ni msukumo wangu unaotokana na dhamira yangu ya dhati ya kuleta aina mpya ya uongozi utakaosaidia kuipeleka nchi mbele zaidi na nimejipanga kushinda.”

Alikutana na wanahabari hao ikiwa ni siku moja baada ya kushiriki mahafali ya 13 ya shule ya sekondari Mtera inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa.

Kuhusu kuwa nyuma ya Lowassa
Makamba alitumia fursa hiyo pia kukanusha uvumi wa baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa wanaodai kwamba anatumiwa kisiasa na Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa anayetajwa pia kuwania nafasi hiyo.

“Mimi ni mtu mzima, nina utashi wangu, nina familia yangu, nina mke na watoto, nina jimbo, nina nyadhifa serikalini na kwenye chama, kuniambia mimi nafanya jambo fulani kwasababu ya mtu fulani ni matusi makubwa sana,” alisema.

Alisema watu wanaosema hayo wanakosea sana na kwa bahati mbaya watu hao hawamjui alivyo hivyo wanapaswa kumuomba radhi.

Makamba ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) alisema; “huo unaweza kuwa mkakati na mbinuchafu za kumpunguzia mtu mwingine nguvu za kisiasa ili watu wanaokuamini wakate tama, hata hivyo huko mbele mambo haya yatajulikana.”

Pamoja na kukanusha kuwa nyuma ya mtu yoyote katika harakati zake hizo, Makamba alisema wapo wengine wanaozihusisha harakati zake za sasa na chaguzi za miaka mingine ijayo jambo ambalo pia si la kweli.

“Ukiingia kugombea nafasi za uongozi halafu hufanyi kwa dhamira ya dhati ya sasa wewe hufai kabisa kuwa kiongozi; hayo mawili nayasikia na naomba watanzania wajue kwamba si ya kweli,” alisema.

Kuhusu uzoefu wa kisiasa
Akizungumzia hoja inayotolewa na baadhi ya wanasiasa wanaodai kwamba ili uwe rais lazima uwe na uzoefu wa miaka mingi wa kisasa, alisema zaidi ya marais waliomaliza muda wao na rais aliyeko madarakani, hakuna mtanzania mwingine anayeweza kujitapa kuwa na uzoefu wa kushika nafasi hiyo nyeti ya nchi.

“Uzeofu wa kisiasa wa miaka mingi?, hiyo sio hoja kwasababu unaweza kuwa na uzoefu lakini ukashindwa kuyafahamu na kuyafanyia kazi matatizo ya wananchi,” alisema.

Alisema zaidi ya Rais wa kwanza Julius Nyerere, wa awamu ya pili All Hassan Mwinyi, wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa na Rais wa awamu hii ya nne Jakaya Kikwete, hakuna mwingine anayeweza kujisifu kwamba ana uzoefu huo.

Akitoa mifano alisema kama uzoefu wa kisiasa kingekuwa kigezo muhimu cha kumpata Rais wa nchi, Mwalimu Julius Nyerere  asingeingia kwenye historia hiyo kwani alichaguliwa kuwashika nafasi hiyo ya uongozi akiwa kijana asiye na uzoefu unaozungumzwa.

“Ipo na mifano mingine ya nje ya nchi. Barack Obama amechaguliwa kuwa Rais wa taifa kubwa kabisa duniani kiuchumi akiwa na uzoefu wa kisiasa wa miaka mitano tu,” alisema.

Alisema ametangaza nia ya kuwania urais wa nchi hii baada ya kujiuliza maswali muhimu matatu, mojawapo likiwa ni kama kazi hiyo utaiweza kwa maana ya kuwa na uwezo wa uongozi, kuwa meneja wa kazi hiyo na kuhamasisha wananchi kuleta maendeleo.

Swali lake la pili, Makamba alisema ni kama anaweza kuwaunganisha watanzania wote bila kujali dini, itikadi wala rangi zao na la tatu kama ana mawazo mapya yanayoweza kusaidia kuleta mabadiliko ya kimaendeleo katika nchi.

“Majibu ya maswali hayo yote ni ndio. Nataka kuona nchi yetu inasonga mbele kwa kasi zaidi. Nina dhamira ya dhati kabisa ya kuleta aina mpya ya uongozi nchini; swali la nne ninalojiuliza ni kama nitaweza kushinda, na swali hil o tunaendelea kulifanyia kazi kwasababu ni lazima ushiriki kwenye mchezo wenyewe.

Kuhusu baadhi ya mikutano ya CCM kukosa mwamko
Alisema sio tu katika mikutano ya kisiasa bali popote pale ambapo kutakuwepo na malalamiko fulani, watu watajitokeza kusikiliza.

“Watu wavivu kusikiliza kile kilichofanywa. Watu wanapenda kusikiliza malalamiko, kwahiyo watu wanakwenda katika mikutano ya upinzani kwasababu wanajua lazima kuna malalamiko,” alisema.

Hata hivyo alisema yapo maeneo ambayo CCM inapata watu wengi katika mikutano yake huku wapinzani wakiambulia patupu kama ambavyo katika baadhi ya maeneo nchini wapinzani nao wamekuwa wakipata watu wengi.

“Uwingi wa watu katika mikutano hakiwezi kuwa kigezo cha mwisho cha kujihakikishia ushindi katika chaguzi kwa kuwa wapo wengi pia ambao hawaendi kabisa katika mikutano hiyo lakini huwa wanafanya maamuzi kwa kutumia sanduku la kura,” alisema.

Kuhusu mchakato wa Katiba
Aliwataka watanzania kujitokeza kwa wingi kuipigia kura ya kuikubali kwasababu Katiba Pendekezwa ina mambo mengi mapya yatakayowasaidia watanzania kwa ujumla wao tofauti na katiba ya sasa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment