Thursday, 30 October 2014

PSPF YAIPIGA JEKI SEKTA YA ELIMU MKOANI IRINGA

Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Gerald Guninita akipokea kutoka kwa Amelia Rweyemamu moja kati ya mabati 200 yaliyotolewa na PSPF kusaidia ujenzi wa maabara unaoendelea katika shule zote za sekondari za wilaya hiyo
Hapa ilikuwa wakati Mwakilishi wa PSPF Mkoa wa Iringa, Baraka Jumanne alipokuwa akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Evalista Kalalu bati 100 zilizotolewa na PSPF kwa ajili ya chuo cha Ualimu Mufindi
Meneja wa Chuo cha Ualimu Mufindi, Erick Ngimba akipokea msaada huo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Evalista Kalalu
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Evalista Kalalu alipokuwa akishukuru kwa msaada huo
Baraka Jumanne wa PSPF alipokuwa akielezea maudhui ya msaada huo
Baadhi ya wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Mufindi wakifuatilia wakati PSPF ikitoa msaada huo
MFUKO wa Pensheni ya Watumishi wa Umma (PSPSF) umetoa msaada wa mabati 300 yenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni sita katika wilaya za Kilolo na Mufindi, mkoani Iringa.

Wakati wilaya ya Kilolo imepata bati 200 zitakazotumika kusaidia kukamilisha ujenzi wa maabara unaoendelea  katika shule zake za sekondari, Chuo cha Ualimu Mufundi kilichopo mjini Mafinga wilayani Mufindi kimepata bati 100.

Mkuu wa wilaya ya Kilolo, Gerald Guninita alipokea bati hizo Jumanne kwa niaba ya wilaya yake, huku Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Evalista Kalalu akipokea bati hizo Jumatano kwa niaba ya chuo hicho.

Katika makabidhiano hayo, PSPF iliwakilishwa na Amelia Rweyemamu kutoka Dar es Salaam na Afisa Mfawidhi wa PSPF Mkoa wa Iringa, Baraka Jumanne.

Akikabidhi msaada huo, Rweyemamu alisema msaada huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya jitihada za mfuko huo kushirikiana na wadau wake kukuza sekta ya elimu nchini.

“Tunatambua agizo la Rais Jakaya Kikwete linalotaka shule zote nchini ziwe zimekamilisha ujenzi wa maabara za fizikia, kemia na baiolojia ifikapo Novemba 31, mwaka huu; kwa mkoa wa Iringa tumetoa msaada wa bati 200 kwa wilaya hii ya Kilolo” alisema.

Na kwa upande wa wilaya ya Mufindi, Afisa Mfawidhi wa PSPF Mkoa wa Iringa, Jumanne alisema PSPF imekisaidia Chuo cha Ualimu Mufindi baada ya kuyazingatia maombi yake yanayolenga kukiboresha chuo hicho binafsi kinachomilikiwa na vijana wawili wajasiriamali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Rweyamamu, PSPF kila mwaka, imekuwa ikiombwa mambo mengi kutoka kwa wadau wake na imekuwa ikiyafanyia kazi kulingana na rasilimali iliyopo.

Akishukuru kwa msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo alisema wilaya hiyo ina shule za sekondari 24 zinazohitaji kuwa na maabara ifikapo Novemba 31 kama ilivyoagizwa na Rais.

“Tunaendelea kutekeleza agizo hilo la Rais kwa kazi kubwa, niwashukuru PSPF kwa mchango huu mkubwa na wadau wengine wote wanaoendelea kutuunga mkono katika harakati hizi za kukamilisha ujenzi huu wa maabara,” alisema.

Alisema bati hizo zitapelekwa katika shule za sekondari mpya zilizojengwa mwaka jana za Kiheka, Ipeta na Lulanzi zilizojengwa mwaka jana.

Kwa niaba ya Chuo cha Ualimu Mufindi, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Kalalu aliishukuru PSPF kwa msaada  wa bati hizo katika chuo hicho.

“Mnatoa msaada miezi michache tu baada ya kutupa msaada mwingine wa zaidi ya madawati 400 kwa ajili ya kusaidia shule zetu za wilaya ya Mufindi,” alisema.

 Aliiomba PSPF iendelee kuisaidia wilaya ya Mufindi katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu na afya.

“Tuko katika mpango wa kuboresha shule zetu ili kuona watoto wetu wanapata elimu stahiki. Pamoja na mchango mkubwa mnaotoa katika sekta ya elimu, tunaomba pia mtusaidie katika sekta ya afya,” alisema.

Meneja na mmiliki wa chuo hicho, Erick Ngimba alisema bati hizo zitatumika kuezekea moja katika ya majengo ya chuo hicho yanayoendelea kujengwa.

Ngimba anayeshirikiana na Peter Chula kuendesha chuo hicho alisema chuo hicho kinachoendelea kujengwa wakati kikiendelea kutumika kinahitaji msaada mkubwa kutoka kwa wadau wake ikiwemo serikali.

“Sisi wenyewe kwa nguvu yetu tumeshawekeza katika chuo hiki zaidi ya Sh Milioni 200. Tumefika hapa tulipo kwa nguvu zetu, tunaendelea kuboresha mazingira ya chuo lakini hatutafanikiwa kama hatutaungwa mkono na wadau,” alisema.


Alisema mbali na jengo la utawala chuo hicho chenye wanafunzi zaidi ya 300 wanaosoma ualimu kwa ngazi ya cheti kina madarasa saba na bweni moja la wanafunzi wa kike.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment