Thursday, 16 October 2014

PROFESA MSOLLA KUCHANGIA UJENZI WA JOSHO KIJIJINI IKUKA

Profesa Peter Msolla alipokuwa akizindua ofisi ya kijiji cha Bomalang'ombe hivikaribuni
MBUNGE wa Jimbo la Kilolo, Profesa Peter Msolla ameahidi kusaidia ujenzi wa josho katika kijiji cha Ikuka kilichopo kata ya Uhambingeto, jimboni humo.

Katika ziara yake aliyofanya hivikaribuni kijijini hapo, Profesa Msolla alisema kwa kupitia mfuko wa jimbo msaada utakaotolewa utahusisha vifaa kama mabati, sementi na misumari.

Alitoa ahadi hiyo akiitikia ombi la wananchi wa kijiji hicho waliosema wana mifugo mingi ambayo iko hatarini kiafya kwasababu ya ukosefu wa josho.

“Asilimia kubwa ya wananchi wa kijiji wanatumia maksai kwa ajili ya kilimo, tunaona umuhimu wa afya ya mifugo yetu, hivyo tunaomba kusaidiwa kujenga josho,” alisema Kaimu Afisa Mtendaji wa Kijiji, Naomi Ngailo.

Pamoja na ombi la ujenzi wa josho, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Amir Mhanga alisema wananchi wa kijiji chake wanasita kuongeza kasi ya kilimo cha mahindi kutokana na ukosefu wa soko.

“Kwasasa gunia moja la mahindi la kilo 100 linauzwa kwa Sh 20,000. Bei hii ni ndogo ukilinganisha na mfuko mmoja wa kilo 50 wa baadhi ya mbolea za viwandani,” alisema.

Alisema ukosefu wa soko na bei ndogo kunawafanya baadhi ya wananchi wanaotegemea kilimo kwa maisha yao ya kila siku kukosa fedha kwa ajili ya kupata mahitaji mengine.

Alimuomba mbunge huyo awasaidie kutafuta masoko ili kuwanusuru na ukata wananchi hao waliomasishwa kuongeza tija katika kilimo.

“Kwanza niwape pole wananchi wote wa jimbo langu na taifa kwa ujumla kwa kukosa soko la uhakika la mazao yao, lakini naomba ieleweke kwamba msimu wa kilimo uliopita ulikuwa wa neema kubwa,” alisema Profesa Msolla.

Alisema neema hiyo ilisababisha uzalishaji mkubwa wa mazao mbalimbali yakiwemo mahindi kila mahali yalikolimwa.

“Serikali inalitambua hilo na inaendelea kulifanyia kazi kwa kuangalia pia masoko nje ya mipaka ya nchi kama Kenya na Sudani,” alisema.

Wakati wakiendelea kusubiri, Profesa Msolla aliwasihi wananchi hao kuhifadhi mazao yao vizuri ili masoko yatakapopatikana yawe katika hali nzuri.

“Msikate tamaa, ongezeni bidii zaidi katika kilimo, msimu uliopita mlipata sana, msimuu huu hatujui nini kitatokea kwasababu sehemu kubwa ya kilimo chetu ni kile kinachotegemea mvua,” alisema.

Katika maombo yao mengine kwa mbunge huyo, wananchi wa Ikuka waliomba msaada wa kukamilisha ujenzi wa zahanati, nyumba ya mwalimu na ujenzi wa barabara ya Ikuka Image kutokana na umuhimu wake kwa watu wapande hizo mbili.

Akizungumzia hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa zahanati, mwenyekiti wa kijiji alisema; “ujenzi huu unaofanywa kwa kutumia nguvu za wananchi unakaribia kufikia hatua ya lenta, tofali 27, 000 zilifyatuliwa wakati mahitaji ni tofali 50,000.”

Reactions:

0 comments:

Post a Comment