Thursday, 16 October 2014

PIGA SIMU YA BURE NAMBA 0800751212 KUFICHUA MAJANGILI


SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa kupitia Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania (SPANEST) limezindua rasmi namba ya simu  itakayowawezesha wananchi kutoa taarifa za ujangili bila kutozwa gharama yoyote.

Mratibu wa SPANEST, Godwell Ole Meing’ataki aliitaja namba hiyo iliyozinduliwa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Dk Leticia Warioba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Christine Ishengoma kuwa ni 0800751212.


Uzinduzi wa namba hiyo ulifanywa katika kijiji cha Kimande, Pawaga kwenye kilele cha fainali za kombe la SPANEST lililoshirikisha timu 21 za vijiji vinavyozunguka hifadhi ya Taifa ya Ruaha vinavyounda Jumuiya ya Wanyamapori Tarafa ya Idodi na Pawaga (Mbomipa).

Meing’ataki alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa zinazohusu mipango au mbinu zinazofanywa na mtu au watu wowote wale kufanikisha ujangili.

“Hata hivyo ni muhimu sana mnapotumia namba hiyo ya simu, msifanye hivyo kwa kutoa taarifa za uongo kwasababu ya chuki au hila mkilenga kuwakomesha wasio na hatia,” alisema.

Alisema ni muhimu taarifa zinazotolewa zikawa ni zile tu zenye ushahidi ili hatua zinapochukuliwa kusiwepo na hoja ya kuonea watu.

Wakati huo huo, Meing’ataki alisema wakati wowote kuanzia sasa tembo wa Hifadhi ya Ruaha wa watafungwa kifaa maalumu cha kufuatilia mwenendo wao, hizo zikiwa ni harakati za ziada za serikali na wadau  za kuwanusuru wanyama hao na majangili wa meno yake.

Bila kumtaja mzabuni atakayefanya kazi hiyo, Meing’ataki alisema mpango huo utakaotumia teknolojia ya kisasa ya mawasiliano ya setilaiti ya utambuzi wa jiografia ya maeneo (GPS) na kompyuta utatekelezwa kupitia SPANEST.
  
“Kwa kupitia mpango huo tembo viongozi wa makundi ya tembo watafungwa kifaa maalumu shingoni kitakachokuwa kinatoa taarifa za mwenendo wao katika kila eneo watakalokuwepo ndani na nje ya hifadhi,” alisema.

Alisema kwa kupitia kifaa hicho askari wa wanyamapori watakabiliana kirahisi na majangili wa meno ya tembo katika azma ile ile ya kunusuru kiumbe hicho kinacholiingizia Taifa mapato makubwa ya kigeni.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment