Thursday, 30 October 2014

NG'OMBE 376 WADAIWA KUPOTEA RANCHI YA RUVU


UPOTEVU wa ng’ombe kwenye ranchi za taifa umeilazimisha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kutoishauri Serikali kutoa fedha Sh bilioni 17 zilizoombwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (Narco) kwa ajili ya kuboresha miundombinu.

Uamuzi wa PAC unatokana na taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) aliyebaini upotevu wa ng’ombe 376 ndani ya miezi mitatu kwenye ranchi ya Ruvu.

Akitoa maagizo kwa Narco, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe alisema “Kamati haiwezi kuitaka Serikali itoe fedha Sh bilioni 17 mlizoomba na tutaenda kusema bungeni kuwa msipewe fedha mpaka hapo mtakapobadilika.

“Upotevu wa kiasi kikubwa cha ng’ombe umefanyika kwenye ranchi moja ya Ruvu, kuna wakati pia ng’ombe 800 walipotea kwenye ranchi ya Kongwa na tungeamua kukagua kwenye ranchi zote hali ingekuwa mbaya,”

Mbali na kukataa Narco kupewa fedha hizo, Filikunjombe pia alitoa wiki tatu kwa Mwenyekiti wa Bodi na Bodi yake kutathmini Menejimenti ya Ranchi ya Ruvu kama inastahili kuendelea kuwapo.

“Umri wa Mkurugenzi wa Ranchi ya Ruvu (Dk John Mbogoma) ni miaka 61 wakati umri wa kustaafu ni miaka 60 sasa Bodi itueleze wanaona ni kwanini aendelee kuwapo,” alisema.

Filikunjombe pia amemuagiza Msajili wa Hazina kufanya tathmini kama Mwenyekiti wa Bodi, Salum Shamte anafaa kuendelea na wadhifa wake huo.
Awali kabla ya kutoa maagizo hayo, Filikunjombe alihoji iweje ng’ombe 376 wapotee katika ranchi moja ndani ya miezi mitatu kama kweli uongozi huo una mfumo wa kuthibiti wizi.

Akijibu hoja hiyo, Mkurugenzi wa Ranchi ya Ruvu Mbogoma, alisema utaratibu uliopo ni kila boma kuna kitabu cha kukabidhiana mifugo na kuwa utawala wake ndio uliobaini upotevu wa ng’ombe hao na kutoa taarifa kwenye vyombo vya usalama.Mwenyekiti wa Bodi Shamte alisema kuwa fedha zilizotoka zilikuwa ni Sh bilioni 5.64 na kuwa waliingia mkataba na SUMA JKT ili kujenga machinjio lakini alilazimika kusitisha kutokana na shirika hilo kujenga chini ya kiwango.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment