Tuesday, 21 October 2014

NDOA YA INSPECTOR HAROUN YATIMIZA MIAKA 10

Inspector Haroun na mkewe
MKONGWE wa muziki wa kizazi kipya nchini, Haruna Kahena ‘Inspector Haroun’ au ‘Babu’ anatarajiwa kufanya shoo ya kuadhimisha miaka kumi ya ndoa yake, itakayofanyika Octoba 25 katika ukumbi wa Mpoafrika Devis Corner, Temeke Dar es Salaam.

Kiingilio katika shoo hiyo iliyopewa jina la ‘Usiku wa Wakongwe’ kitakuwa sh 5,000 na itaanza saa mbili usiku na kuendelea ambapo atasindikizwa na wakongwe kibao.

Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Inspector alisema kuwa, anaomba mashabiki wa muziki wake wamwagike kwa wingi katika ukumbi huo kwa lengo la kupata burudani ilikwenda shule.

Alisema atasindikizwa na Luten Karama, TID Mnyama, Scorpion Giirlz (Isabela), LWP & Mabaga Flesh, Young Tuso & Drama Boy na Kimbiza Dj’s.

Inspector alisema kuwa siku hiyo atafanya shoo kubwa ambayo hajafanya kwa muda mrefu hivyo wapenzi wa kazi zake wanatakiwa kumwagika kwa wingi.

Mkongwe huyo alishawahi kutamba na ngoma zake kama Asali wa Moyo, Sharubu za Babu, Mungu ndio anapanga na nyingine nyingi ambazo zilimtambulisha na kufanya vizuri katika tasnia ya muziki huo.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment