Sunday, 26 October 2014

MILIONI 700 ZATUMIWA NA HALMASHAURI YA WILAYA YA IRINGA KUNUNUA GREDA LA KISASA

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa (mwenye gauni jekundu) akiwa na maafisa wa halmashauri na wawakilishi wa kampuni ya MACS Ltd mbele ya mtambo wa kuchonga barabara walioununua kutoka katika kampuni hiyo kwa Sh Milioni 700
Mwakilishi wa kampuni ya MACS Ltd akimkabidhi funguo za greda hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Pudenciana Kisaka ikiwa ni ishara ya makabidhiano ya mtambo huo
Pudenciana Kisaka, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa akijaribu kuwasha greda hilo, anayeengalia ni mwakilishi wa kampuni ya MACS Ltd,  Edson Nalogwa wasambazaji/wauzaji wa mitambo hiyo
Greda hilo linavyoonekana
HALMASHAURI ya wilaya ya Iringa imetumia zaidi ya Sh Milioni 698.3 kununua mtambo wa kisasa wa kuchonga barabara (motor grader) ambao mbali na kutumiwa kwa kazi za halmashauri hiyo, utakodishwa kwa wakandarasi mbalimbali.

Mtambo huo ulionunuliwa kutoka katika kampuni ya Mining Agriculture & Construction Services Ltd (MACS) yenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam, ulikabidhiwa juzi kwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Pudenciana Kisaka.

Mwakilishi wa MACS, Edson Nalogwa alisema wakati wa makabidhiano hayo kwamba jukumu kubwa la mtambo huo uliotengenezwa nchini Marekani ni toleo jipya aina ya 772G na mpya katika soko la Tanzania.

Alisema mbali na kampuni yao ya MACS kujishughulisha na uuzaji wa mitambo ya barabara, inajishughulisha pia na uuzaji wa mitambo ya kilimo, migoni na ujenzi.

Alisema kampuni hiyo inasambaa kwa kasi nchini kote na imekwishafungua matawi ya kiufundi katika mikoa ya Iringa (Mafinga), Mbeya (Chunya), Shinyanga (Mwadui) na Morogoro (Kilombero).

Awali Mkurugenzi wa halmashauri hiyo alisema; “greda hilo limenunuliwa kupitia utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika sekta ya ukusanyaji wa mapato.”

“Tukiendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato, tulianza na kujenga jengo la vyumba vya biashara lililopo mkabala na stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani, tukajenga mgahawa uliopo pembeni mwa ofisi yetu na sasa tumenunua greda hili,” alisema na kuongeza kwamba miradi yote hiyo itasaidia kuiongezea halmashauri hiyo mapato.

Alisema wameweza kununua greda hilo baada ya benki ya CRDB tawi la Iringa kukubali kuwapa mkopo wa Sh Milioni 458.2 huku wao wenyewe kwa kupitia vyanzo vyao vya mapato ya ndani wakitoa Sh Milioni 240.1.

Kisaka alisema mtambo huo utakuwa ukikodishwa kwa wakandarasi mbalimbali na hivyo kuwaongezea mapato, na watautumia kuboresha na kuchonga barabara mpya katika halmashauri hiyo ili kuchochea shughuli za uchumi ikiwemo kilimo.

Alisema  baada ya kuupokea kutoka kwa wawakilishi wa kampuni hiyo, mtambo huo utakabidhiwa rasmi kwa Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo, Oktoba 31, mwaka huu.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment