Monday, 27 October 2014

KUNA NINI IRINGA BAADA YA LAAC KUMALIZA KUKAGUA HESABU ZA HALMASHAURI

Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabau za Serikali za Mitta

KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) leo inamaliza kukagua hesabu za halmashauri zote za mkoa wa Iringa.

Ilianza Kilolo, ikaja Iringa Vijijini, ikaenda Mufindi na leo inamalizia kukagua hesabu na baadhi ya miradi iliyotekelezwa na halmashauri ya manispaa ya Iringa.

Mengi mabaya yameibuka katika halmashauri hizo, siyasemi hapa leo, lakini yataletwa kwako muda si mrefu kupitia mtandao huu na vyombo vingine vya habari.

Jambo la kusikitisha katika shughuli hiyo ni kwamba zipo baadhi ya halmashauri hazitaki kuwaalika wanahabari hasa wale wenye uwezo wa kuandika habari zinazotaka kufichwa na halmashauri hizo.

Katika halmashauri hizo, yapo madudu ambayo kama yataanikwa hadharani hakuna ubishi kwamba wanaohusika wanaweza kuwajibishwa ikiwa ni pamoja na kufikishwa kwenye vyombo vya dola.

Nitumie fursa hii kupeleka lawama zangu kwa zile ofisi katika halmashauri hizo zilizoanzishwa kwa lengo la kurahisisha wanahabari na vyombo vyao vya habari wapate taarifa muhimu za halmashauri hizo kwa ajili ya kuulisha umma.

Baadhi ya ofisi hizo, nadiriki kusema hivisasa zimegeuzwa kuwa vichaka vya kuficha maovu ndani ya halmashauri zao; na kwa hakika zinatumika kwa makusudi kabisa kuwanyima mialiko baadhi ya wanahabari wenye uwezo wa kujenga mashaka (nitakuja kukutajia maafisa habari hao, naendelea kukusanya ushahidi)

Katika halmashauri hizo kuna Mashaka ya kuwepo kwa matumizi mabaya ya madaraka, mashaka ya kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha za umma, mashaka ya kuwepo kwa vitendo vya rushwa, mashaka ya kutisha watu wasiseme yale mabaya wanayojua kuhusu wakubwa zao, mashaka ya kutotimiza wajibu, na mashaka ya matumizi mabaya ya rasilimali za umma yakiwemo magari ya serikali (leo hii tunaona baadhi ya magari ya serikali mpaka usiku wa manane yakiwa kwenye vilabu vya pombe).

Mashaka mengine ni ya upendeleo na yale ya kuwapa wasiohusika kazi za wafanyakazi wa idara zingine (tunaambiwa wapo wanaotumiwa kwenye manunuzi ya halmashauri wakati kazi hizo si zao), mashaka ya upendeleo wa aina mbalimbali na mashaka mengine mengi yanayofanana na hayo.

Baadhi ya maafisa habari hao (nitakutajia kwa majina) wamekuwa mihuri ya wakubwa. Wanaficha mashaka yote hayo yasijulikane; huenda wanafanya hivyo kwa mishahara yao ile ile wanayoilalamikia kila siku lakini huenda wanapata nyongeza.

Nyongeza inayotoka na mgao wa uwepo wa mashaka hayo; tumefanya kazi kubwa lakini bado hatujafika safari tunayotaka kwenda.

Safari hii kwa wanahabari wenzangu ni ndefu sana, tubadilike sasa, tuanze kuusaidia umma kupata kile wanachohitaji kupata, kupata zile habari zinazofichwa na wakubwa pamoja na maafisa habari hao, kupata zile habari zitakazowakasilisha baadhi ya watu lakini zitakazobadili mwelekeo wa taifa hili na kuleta neema kwa watanzania wengi.

Kila mwanahabari aseme SASA KAZI NDIYO IMEANZA NIPE TAARIFA NIKUHAKIKISHIA NITAIFANYIA KAZI NA MATOKEO YAKE UTAYAONA….

Itaendelea…………………….


Reactions:

0 comments:

Post a Comment