Tuesday, 21 October 2014

KATIBA INAYOPENDEKEZWA KUPIGIWA KURA MACHI 30, 2015


Kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa itafanyika Machi 30 mwakani, gazeti hili limethibitisha.

Hayo yalisemwa jana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema ambaye hata hivyo, alimwambia mwandishi wetu kwamba kabla ya kura hiyo, “lazima daftari la kudumu la wapigakura liboreshwe kwanza” ili kuwapa fursa wapigakura wapya ambao hawamo kwenye daftari hilo.

“Kuboreshwa kwa daftari la wapigakura ni lazima kwa sababu kuna watu wengi wamefikisha umri wa kupiga kura tangu tulipofanya uchaguzi mkuu na hawamo kwenye daftari hilo, kwa hiyo hatuwezi kuwanyima fursa ya kupiga kura kwa sababu ni haki yao kikatiba,” alisema Jaji Werema na kuongeza;

“Lakini lazima tujue pia kwamba kuboreshwa kwa daftari hilo kunahitaji fedha, kwa hiyo kuboreshwa kwake kutategemea kama Serikali itatoa fedha kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kazi hiyo iweze kufanyika, tusipoboresha daftari tutasababisha kelele na malalamiko mengi”.

Msimamo wa Jaji Werema ni sawa na ule wa Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva ambaye amesisitiza mara kadhaa kwamba tume yake haitoandaa uchaguzi wowote pasipo daftari la kudumu la wapigakura kuandikwa upya.

Jaji Werema alisema ikiwa Serikali itatoa fedha, uboreshaji wa daftari unaweza kukamilika ifikapo Februari 2015 na kwamba inatarajiwa kwamba Machi 30, mwakani kura ya maoni itapigwa kama kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa.

Alisema upigaji kura utatanguliwa na kampeni ambazo zitafanyika kwa siku 30 kuanzia mwanzoni mwa Machi ili kushawishi Katiba inayopendekezwa iungwe mkono au kinyume chake kwa makundi yanayoipinga.

Hadi sasa gharama za kusimamia kura ya maoni kwa ajili ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa zimeendelea kuwa kitendawili.

Jana, Jaji Lubuva alisema asingeweza kuzizungumzia kwa kuwa yuko Dodoma kikazi na kuelekeza taarifa hizo zinaweza kupatikana kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Julius Malaba.

Hata hivyo, alipotafutwa Malaba alisema anaweza kuzungumzia suala hilo katika mkutano na waandishi wa habari anaotarajia kuuitisha wiki hii.

“Wiki hii nitaitisha mkutano na waandishi wa habari kuhusu daftari la wapigakura. Nadhani itakuwa vyema suala hilo likiibuliwa kupitia mkutano huo ndipo majibu yanapoweza kupatikana,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment