Thursday, 30 October 2014

HUKUMU YA MWENYEKITI ALIYETISHIA KUMUUA MBUNGE WA ZAMANI WA NJOMBE MAGHARIBI NOVEMBA 27

Yono Kevela
HUKUMU ya kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya
Wanging’ombe, Anthony Mahwata ya kutishia kumuua kwa maneno Mbunge wa zamani wa Jimbo la Njombe Magharibi, Yono Kevela imepangwa kuwa Novemba 27, mwaka huu.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Njombe, Augustino Rwizile juzi alitaja tarehe ya hukumu hiyo baada ya kusikiliza ushahidi wa utetezi wa upande wa washtakiwa waliokuwa wameletwa mahakamani hapo kufuatia Mahwata na mwenzake Evaristo Makurumbi kuomba kuleta mashahidi wao juzi mahakamani.

Mashahidi waliofika mahakamani na kutoa ushahidi wao ni Pascal Mahwata ambaye ni mdogo wa mwenyekiti huyo, Malumbu Kihwele ambaye ni dereva wake na Malumbu Mligo, nahodha wa timu ya soka ya Igwachanya B.

Katika kesi hiyo, Mwenyekiti Mahwata na Makurumbi wanashitakiwa na Jamhuri kwa kutishia kumuua kwa maneno Yono na pia kusababisha uvunjifu wa amani wakati timu ya Yanga Veteran ya Dar es Salaam ilipokwenda kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya soka ya Igwachanya, katika Kijiji na Kata ya Igwachanya, kwa mwaliko wa Chama cha Soka cha Wilaya ya Wanging’ombe.

Awali wakati kesi hiyo iliposikilizwa Oktoba 23, mwaka huu, mshitakiwa Mahwata aliiomba mahakama ikubali atoe vielelezo vya magazeti, ujumbe wa simu ya mkononi (sms) na taarifa za kwenye mitandao ya kijamii aliodai umekuwa ukitumiwa na Yono kumchafua kisiasa, ombi ambalo halikukubaliwa na Hakimu Rwezila.

“Mheshimiwa Hakimu, mashahidi mbona wanatengenezwa, Yono anatengeneza ushahidi wa uongo ili kuniharibia kisiasa, mashahidi wote ni wa kutengenezwa hawana kumbukumbu,” alisema Mahwata wakati alipopanda kizimbani.

Akitoa ushahidi wake Kihwele ambaye ni dereva wa gari namba T749 AYU aliyedai ana uzoefu wa kuendesha gari na pia anayo leseni halali kwa kipindi cha miaka mitano, alitoa maelezo yenye kujikanganya baada ya kuulizwa kama ana kumbukumbu sahihi za namba ya gari anayoiendesha.

Huku akiwa hana kumbukumbu ya namba hiyo, shahidi huyo alilazimika kuangalia kiganjani kwake alipokuwa ameiandika namba hiyo, na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Atu Mwakasitu aliiomba mahakama imwamuru shahidi huyo aoneshe kilichoandikwa kiganjani, ambapo alinyoosha mkono uliokuwa umeandikwa namba hiyo.

Awali akisoma mashtaka dhidi ya washtakiwa hao, Mwendesha Mashtaka Mwakasitu alisema kuwa Februari 5, 2013, Mahwata na Makurumbi wakiwa katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Igwachanya na baadaye kwenye Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Kijiji cha Igwachanya walihatarisha uvunjifu wa amani.Alisema hatua hiyo ilitokana na kuweka magari yao mawili aina ya RAV 4 namba T 749 AYU na Noah namba T 973 BGG katikati ya magoli kwa lengo la kuzuia mchezo huo usichezwe, na baadaye kutishia kumuua kwa maneno Yono.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment