Monday, 27 October 2014

DIWANI, WANA CCM WAJITOLEA KUJENGA MAABARA YA SHULE YA SEKONDARI MIYOMBONI

Jesca Msambatavangu akichimba msingi wa maaba ya sekondari Miyomboni
Wengine walikuwa wakisogeza mawe
Huku wengine wakichimba
Kila mmoja alikuwa na la kufanya katika azma yao ya kuchangia ujenzi wa maabara ya shule hiyo
DIWANI wa kata ya Miyomboni mjini Iringa, Jesca Msambatavangu na wanachama wenzake wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamejitolea kujenga maabara katika shule ya sekondari ya kata hiyo ya Miyomboni.

Ujenzi wa maabara hiyo kwa mujibu wa Msambatavangu ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Iringa ni utekelezaji wa agizo la ujenzi wa maabara katika shule zote za sekondari nchini lililotolewa na Rais Jakaya Kikwete Julai mwaka huu.

Akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Tanga, Rais Kikwete aligiaza shule zote za sekondari ziwe na maabara kwa ajili ya masomo ya sayansi ifikapo Novemba mwaka huu.

Rais Kikwete aliwaagiza wakuu wa mikoa na wilaya washirikiane na wananchi katika maeneo yao kuhakikisha shughuli hiyo inakamilika ifikapo mwezi huo.

Katika kuitikia agizo la Rais, Msambatavangu na baadhi ya wananchama wa CCM wa kata hiyo juzi saa 12.00 asubuhi walikusanyika katika shule hiyo na kuanza kutekeleza ahadi yao ya ujenzi wa maabara katika shule hiyo.

Wanahabari waliokuwepo waliwashuhudia wanaCCM hao wakisogeza mawe katika eneo la ujenzi huku wengi wakichimba msingi wa chumba hicho cha maabara na baadaye kuanza kujenga.

Msambatavangu alisema; “tumenunua mawe, tumeahidiwa kupata tofali na tunachimba na kujenga msingi ikiwa ni ishara ya kuzindua ujenzi wa maabara ya shule hii.”

Alisema kwa kuwa wamaechelewa kuanza ujenzi huo watahakikisha ujenzi wa maabara hiyo unakamilika ifikapo Desemba mwaka huu na kuikabidhi kwa uongozi wa shule.

Aliwataka wanachama wa CCM na viongozi wao wote katika kata zote za mkoa wa Iringa kushiriki katika shughuli hiyo muhimu ya maendeleo ya elimu kama ilivyoagizwa na Rais.

“Kwa kufanya hivyo tutakuwa pia tunaitikia wito wa Katibu Mkuu wa CCM Abdulahman Kinana anayeonekana mara kwa mara akishiriki shughuli za maendeleo katika ziara zake nyini za kikazi anazofanya nchini,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment