Friday, 17 October 2014

CHADEMA YAANZA KAMPENI YA KUKATAA KATIBA NCHI NZIMAhttp://freemedia.co.tz/daima/wp-content/uploads/2014/04/slaa.jpg
Dk Slaa


LEO Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza kuanza rasmi kampeni ya nchi nzima ya kuwashawishi Watanzania, kuhakikisha katika uchaguzi wa kura ya maoni ya kuipigia Katiba Inayopendekezwa, kura ya hapana.

Aidha, chama hicho kimebainisha kuwa kinakutana na vyama vingine vya siasa vya upinzani vilivyopo kwenye kundi la Umoja wa Katiba ya Watanzania (UKAWA) kwa ajili ya kuangalia namna ya kushirikiana katika kampeni hiyo na Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willbrod Slaa alisema kwa kuanzia, wataanza kampeni ya siku 20 itakayoongozwa na Baraza la Wanawake Chadema (Chadema) chini ya Mwenyekiti wao, Halima Mdee.

Alitaja maeneo ambayo kampeni hizo zitaanza kuwa ni Mwanza, Ukerewe, Magu, Sengerema, Geita, Busanda, Bukombe, Karagwe, Chato, Biharamulo na Shinyanga mjini.

“Haya ndio maamuzi ya Kamati Kuu juu ya Katiba Inayopendekezwa iliyopitishwa hivi karibuni na Bunge Maalumu la Katiba. Kamati pia imewaagiza viongozi wetu wote wa mikoa, wilaya, kanda, kata, mitaa, vitongoji, vijiji na msingi kuhakikisha wanashiriki ipasavyo katika kampeni hii, na mada kuu ni Katiba hii na suala la uchaguzi wa serikali za mitaa,” alisisitiza.

Aidha, Dk Slaa alizungumzia suala la uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika nchini Desemba 14, mwaka huu, ambapo alibainisha kuwa chama hicho kimejipanga kushiriki kikamilifu kwa kuhakikisha wanabana maeneo yote ili kukipatia ushindi chama hicho.

Alisema viongozi wote wa chama hicho watapimwa ili kuona namna walivyosimamia uchaguzi huo na watakaoshindwa kutimiza wajibu wao watashughulikiwa kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.

Naye Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu alisema kamati kuu ya chama hicho imekitaka chama hicho kuanzia sasa kuacha kulala na badala yake kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa lakini pia wanahamasisha kura ya hapana katika uchaguzi wa kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa.

“Kamati kuu katika kikao chake imeamua kuwa chama chetu hakiitambui Katiba

hii pendekezwa kutokana na mambo mengi ikiwemo, ubabe uliotumika kupatikana, udanganyifu katika kupatikana kwa theluithi mbili ya Zanzibar na bara na kubadilishwa kabisa kwa rasimu iliyopendekezwa na wananchi,” alisema.

Alisema Chadema inatambua kuwa mustakabali wa Katiba mpya nchini hautaamuliwa mahakamani bali utaamuliwa mitaani ambako chama hicho, kimejipanga kuhakikisha wananchi wanaikataa katiba hiyo pendekezwa.

Kwa upande wake, Msemaji wa chama hicho, Tumaini Makene, alisema tayari Chadema imeomba vibali vya kuendesha mikutano hiyo ya hadhara na wanatarajia kupatiwa ulinzi kama inavyofanyika katika mikutano ya vyama vingine vya sias

Reactions:

0 comments:

Post a Comment