Sunday, 26 October 2014

CCM YAZOA WANACHAMA WAPYA 110 KATIKA MKUTANO WAKE WA STENDI YA MLANDEGE IRINGA

Hivi ndivyo mkutano huo wa CCM stendi ya Mlandege ulivyokuwa
Sehemu ya vijana 110 waliojiunga na CCM jana
Kulikuwa na hamasa toka kwa wanachama na wapenzi wa chama hicho baada ya kupokea wanachama hao wapya
Furaha ilikuwa namna hiyo
Katibu wa CCM wilaya ya Mufindi, Miraji Mtaturu kwa niaba ya chama hicho wakaliwezesha kwa Sh 500,000 tawi jipya la VETA ili ziwasaidie kwenye shughuli zao za kijasiriamali
Na tawi la mataxi driver wa stendi ya Mlandege nao wakawezeshwa Sh 500,000
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu akamtambulisha mmoja wa makada wao wa Chuo Kikuu cha Mkwawa
Hapa akimtambulisha Bi Marium wa Chuo Kikuu cha Tumaini
Baadhi ya viongozi waliohutubia mkutano huo
KIKIENDELEA kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa Desemba mwaka huu, Chama cha Mapinduzi (CCM) Iringa Mjini kimenufaika kisiasa baada ya juzi kupata wanachama wapya 110.

Wanachama hao vijana, baadhi yao wakitokea katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) cha mjini Iringa, walikabidhiwa kadi zao na kuapa kuwa waaminifu katika chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa stendi ya mabasi yaendayo vijijini ya Mlandege.

CCM iliamua kuutumia uwanja huo kikilenga kupima mwitikio wa wanachama na wapenzi wake ikiwa ni takribani wiki moja tu tangu viongozi wa kitaifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwemo Dk Wilbroad Slaa kufanya mkutano wao katika uwanja huo huo.

Idadi ya watu waliojitokeza katika mkutano huo ilielezwa na Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Iringa, Abeid Kiponza kwamba ni ya kuridhisha pamoja na kwamba ulihutubiwa na viongozi wa mkoa na wilaya tofauti na ule wa Chadema uliohutubiwa na viongozi wa kitaifa.

Baada ya wanachama hao wapya kuapishwa, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Mufindi, Miraji Mtaturu alikabidi Sh 500,000 kwa wanachama hao wanaounda tawi la VETA.

“Huu ni mchango wa CCM kwa tawi lenu jipya, kama mlivyoainisha kwenye risala yenu, ni matarajio yetu kwamba mtatumia fedha hizo kuanzisha shughuli itakayowahamasisha muwe wajasiriamali,” alisema.

Pamoja na tawi hilo kuchangiwa Sh 500,000; tawi la CCM la Mlandege linaloundwa na madereva taxi nalo lilikabidhi na katibu huyo Sh500,000.

“Haya ndio mambo ya CCM, tunaisimamia serikali kutekeleza Ilani na wakati huo huo tunachangia shughuli za maendeleo za wadau wetu wote na wakati mwingine bila kujali itikadi za siasa, tumefanya hivyo sehemu nyingi na tutaendelea kufanya hivyo” alisema Mtaturu.

Mtaturu alisema siasa ni maisha ya watu na kwa kupitia Ilani ya CCM serikali imeendelea kuzipatia suluhu kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Katika mkutano huo Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi alielezea kazi mbalimbali zilizotekelezwa na halmashauri yake kupitia Ilani ya CCM.

“Tumefanya mengi katika sekta ya afya, elimu, barabara, umeme, maji, biashara, ujenzi na nyingine nyingi. Nyie ni mashahidi,” alisema.


Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu alitoa ufafanuzi wa vifungu mbalimbali likiwemo suala la muundo wa serikali na sifa za kupata wabunge na mawaziri kupitia Katiba Inayopendekezwa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment