Friday, 24 October 2014

CCM MKOA WA IRINGA YAKANUSHA TAARIFA ZA MITANDAONI DHIDI YA CHADEMA, KUFANYA MKUTANO WA HADHARA KESHO

Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa Hassana Mtenga
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa kimekanusha taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinazoonesha kuwahamasisha wanachama wake kuwafanyia vurugu wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassana Mtenga amesema; “Moja ya nguzo kuu ya CCM ni umoja, amani, upendo na mshikamano.”

Mtenga amesema hayo wamekuwa wakiyahubiri kila siku na wataendelea kufanya hivyo kila watakapopata nafasi kwasababu wanafahamu athari za machafuko kwa kuangali kile kilichotokea na kinachoendelea kutokea katika nchi jirani.

Amesema watu wasiokitakia mema chama hicho wamenukuu taarifa potofu na kuisambaza mitandao ikiwaamuru wanachama wa chama hicho kuwapiga na hata kuwatoboa macho wana Chadema.

“Huu ni uzushi mkubwa, uzushi unaotia aibu, uzushi usiopaswa kuvumiliwa hata kidogo kwasababu unalenga kuhatarisha usalama wa wanachama wa vyama hivi viwili kwa maslai ya watu wachache,” alisema.

Mtenga amesema CCM na Chadema vitashindana kwa hoja kwa kuzingatia kwamba hiyo ndiyo demokrasia yenyewe.

Wakati huo huo, Chama hicho kimetangaza kufanya mkutano wa hadhara kesho jumamosi katika uwanja mpana wa stendi ya mabasi ya vijijini ya Mlandege, uliotumiwa hivi karibuni na viongozi wa kitaifa wa Chadema.

Mtenga amewataka wakazi wa manispaa ya Iringa na vitongoji vyake, wapenzi na wanachama wa chama hicho, na wapenzi na wanachama wa vyama vya upinzani kujitokeza kwa wingi kusikiliza mapigo yao ya kisiasa dhidi ya Chadema.

Mkutano huo utakaohutubiwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho utaanza saa nane mchana.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment