Monday, 8 September 2014

WALIMU WANAODAI KUWATIKISA WAKURUGENZI WA HALMASHAURI ZAO SEPTEMBA 15

Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Iringa, Stanslaus Mhongole na Katibu wake, Mshamu Mohamed Mshamu
SEPTEMBA 15 mwaka huu imetangazwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) mkoa wa Iringa kwamba itakuwa siku ya walimu wanaoidai serikali kukusanyika kwa wakurugenzi wa halmashauri za wilaya zote kuthibitisha kile wanachodai.

“Hatutakwenda kazini, kazi yetu itakuwa moja tu kukusanyika kwenye ofisi za wakurugenzi ili kuithibitishia serikali fedha tunazowadai,” alisema Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Iringa, Stanslaus Mhongole.

Akizungumza na wanahabari jana, Mhongole alisema CWT taifa imetoa siku 14 kwa serikali kufanya uhakiki wa madeni ya walimu na kuyalipa baada ya kuwepo na taarifa zinazowachanganya toka serikalini.

Katika taarifa zake nyingi, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amenukuliwa akiuthibitishia umma kwamba zipo dalili za uchakachuaji wa madeni ya serikali.

Akiwa mjini Iringa hivikaribuni, Nchemba alisema serikali italipa madeni yote lakini baada ya kufanya uhakiki na wakigundua kwamba yaliongezwa, mhasibu na mkaguzi wa hesabu waliopitisha madai hayo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Mwenyekiti wa CWT alisema madai ya serikali kwamba yako baadhi ya madeni yaliyochakachukuliwa yanaweza kuwa kweli na wao wako tayari kutoa ushahidi wa mbinu zinazotumiwa na watendaji wa halmashauri kuongeza madeni hayo.

“Tunajua ujanja wa viongozi wetu wa halmashauri na jinsi wanavyotumia ulaghai kuongeza madeni. Watu hao wapo na wanajulikana, serikali haina sababu ya kuzunguka mbuyu, tukae nao tutawaeleza,” Mhongole alisema.

Alisema badala ya mawaziri wa wizara ya fedha kuendelea kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu kuwepo kwa madeni feki ni vizuri wakakaa na viongozi wa vyama vya wafanyakazi kwasababu wanajua mianya inayotumiwa na wajanja katika halmashauri zao.

Ili kuondoa utata unaohisiwa na serikali, Mhongole alisema; “ni vizuri walimu wote wanaodai, wakiwa na orodha ya madai yao, wakaenda kwa wakurugenzi na kuthibitisha kile wanachodai.”

Katibu wa CWT Mkoa wa Iringa, Mshamu Mohamed alisema walimu mkoani hapa wanaidai serikali zaidi ya Sh Milioni 871 ikiwa ni malimbikizo ya mishahara, likizo, uhamisho na madaraja.

Kwa pamoja waliwataka walimu wenye madai yao kuitimia siku hiyo (Septemba 15) kuithibitishia serikali madai yao.

“Ikiwezekana mlale pale pale, tunataka haki za walimu zipatikane; tunataka serikali itemize wajibu wake na iache kuyafanyia kazi mambo baada ya kusikia matamko au baada ya kutokea kwa misukosuko,” Mshamu alisema.

Katika hatua nyingine CWT mkoani hapa imeunga mkono tamko wa CWT Taifa na Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU) linalopinga mpango wa serikali wa kupunguza mafao ya wastaafu kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii.


CWT mkoani hapa imesema mpango huo hauna nia njema kwa hatma ya watumishi wa serikali waliovuja jasho lao kwa muda mrefu kwa maendeleo ya nchi huku wakikubali kulipwa mishahara midogo isiyokidhi haja na wakati huo huo kukubali kukatwa sehemu ya mishahara hiyo na kuiwekeza katika mifuko hiyo kwa manufaa yao pindi wanapostafu.

Reactions:

1 comments:

  1. Liwe zoezi la nchi nzima sio iringa pekee.cwt maeneo mengine mnafanya nini?

    ReplyDelete